TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri [Translation]
Dhana ya Tafsiri.
Tafsiri
 imefasiliwa kuwa, ni Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha
 nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002: 271]
Catford
 [1965:20] anasema tafsiri ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi 
kutoka lugha moja {lugha chanzi} na kuweka badala yake mawazo 
yanayolingana katika lugha nyingine {lugha lengwa}.
Vilevile imefasiliwa kuwa ni “Mawazo yaliyotolewa kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.”
 TUKI [2002: 271] Tafsiri ni kueleza maana ya maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Maana zote hizo tulizoziangalia, utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu yanayojitokeza, mambo hayo ni: 
(i) Mawazo yanayotakiwa kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.
(ii) Mawazo au ujumbe kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
(iii) Tafsiri inaweza kuwa kutoa maana ya maneno au mawazo.
Baada ya kuangalia maana ya tafsiri, sasa tuangalie maana ya mfasiri na sifa anazotakiwa kuwa nazo mfasiri:
Mfasiri
Mfasiri ni mtu anayefanya tafsiri kutoka lugha moja hadi lugha nyinge.[TUKI:2000:165]
Kwa
 ujumla tunaweza kusema kuwa, mfasiri ni mtu anayehamisha mawazo kutoka 
lugha moja (lugha chanzi) kwa kutumia lugha nyingine ili mawazo hayo 
yaeleweke na watu wasiojua au kuielewa lugha chanzi, na mawazo hayo 
sharti yawe katika maandishi.
 Sifa za mfasiri bora
Mfasiri bora anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
? Awe na ujuzi wa lugha fasaha, hii ina maana kuwa awe anajua kwa ufasaha lugha zote mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa.
?
 Awe na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini 
chanzi na uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha 
katika lugha lengwa.
? Awe amesoma maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga halafu aweze kuyafikiria katika lugha lengwa.
 Historia ya Tafsiri nchini Tanzania / Afrika mashariki
Taaluma
 hii ya tafsiri ina historia ndefu hapa dunia tangu kale, lakini kwa 
hapa Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla historia hii ya tafsiri 
haina historia ndefu kwani inaanzia karne ya 19 ambapo wamisionari 
walitafsiri vitabu mbalimbali vya kikristo ikiwemo biblia kutoka lugha 
ya kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila makubwa 
nchini Tanzania.
Na hata wakati wa utawala wa kikoloni 
hasa waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya taaluma na fasihi ya 
Ulaya kwa lugha ya Kiswahili Na hata baada ya uhuru wapo wazalendo 
waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili 
mfano mzuri ni Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere 
ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa
 Uingereza William Shakespeare ambavyo ni: Juliasi Kaizari [1963] na 
Mabepari wa Venisi[1969] {Tazama pia Mwansoko na wenzake 2006 : 5}
Mfano
 wa tafsiri ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ni pamoja na 
ya,Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa ambayo imetafsiriwa na Abdilatif 
Abdalla, House boy ya Ferdinand Oyono iliyotafsiriwa na Raphael Khasao 
na Nathan Mwele. Juliasi Kaizari na Mabepari wa Venisiza zaWilliam 
Shakespeare zilizotafsiriwa na Julius K. Nyerere, Hekaya za Abunuwasi, 
Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa, Alfu 
Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton na Mashimo ya Mfalme 
Suleiman kilichotafsiriwa na Sir Rider Haggard, Takadini,kimetafsiriwa 
na Mathews Bookstore and Stationers, Nitaolewa Nikipenda ambacho 
kimetafsiriwa na Crement M. Kabugi. vitabu vingine vilivyotafsiriwa ni 
kama vile; Orodha, Barua Ndefu Kama Hii n.k.
Mpaka sasa wataalamu
 mbalimbali wamekuwa wakiendelea kutafsiri maandiko mbalimbali kama vile
 mikataba na ripoti mbalimbali za kimataifa, sheria ambazo mwanzo 
zilikuwa zikiandikwa kwa lugha ya kiingereza, vitabu vya kiada na ziada,
 kazi za kifasihi, n.k 
Mambo ya kuzingatia katika tafsiri
Katika
 sehemu hii tutaangalia mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika 
tafsiri, hivyo basi, tutagawa mambo hayo ya kuzingatia katika sehemu 
mbili, sehemu ya kwanza ni mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato 
wa kutafsiri na sehemu ya pili, tutaangalia mambo muhimu ya kuzingatia 
wakati wa mchakato wa kutafsiri. Tukianza na: 
[a] Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri. 
? Kwanza unatakiwa kusoma matini nzima.
Mtu
 anayetaka kutafsiri matini yoyote ile jambo la msingi la kuzingatia ni 
kuisoma matini nzima tena kwa umakini ili kuelewa maudhui ya matini 
chanzi, kuweka alama sehemu za matini zenye utata au zisizoeleweka 
vizuri, hii itamsaidia kubaini ni aina gani ya marejeo muhimu 
yatakayomsaidia kutafsiri mfano wa marejeo hayo ni kama kamusi, 
ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya. 
 
? Unatakiwa kubaini lengo la matini chanzi
Baada
 ya kuisoma matini chanzi, je! Umeweza kubaini lengo la matini chanzi ni
 nini? Kubaini lengo la matini kutakusaidia kuweza kutafsiri bila 
kutofautiana/kukinzana na lengo la matini chanzi, mathalani, matini 
mbili tofauti zinaweza kueleza jambo lilelile na kutumia data zilezile 
lakini mtindo wa lugha uliotumika unaweza ukaonesha mitazamo miwili 
tofauti. 
Hebu angalia tamthilia ya Mercant of Venice, 
iliyoandikwa na William Shakespeare na kutafsiriwa na Mwalimu J.K. 
Nyerere kwa lugha ya Kiswahili na kuitwa Mabepari wa Venisi, kumbuka 
kuwa tamthiliya hiyo ingeweza kuitwa pia Wafanyabiashara wa Venisi 
lakini ukiangalia tafsiri ya kwanza [Ya Mwalimu Nyerere] inatupa hisia 
hasi wakati ya pili huwezi kupata hisia yoyote.{Mwansoko na wenzake 
2006:15} 
? Unatakiwa kubaini hadhira/ wasomaji lengwa.
Kabla
 ya mfasiri hajabaini wasomaji au hadhira ya wasomaji wa matini yake ya 
tafsiri ni vema kwanza akaibaini hadhira ya matini chanzi na ndipo 
abaini hadhira/ wasomaji mahususi wa matini yake ya tafsiri, maswali 
anayotakiwa kujiuliza mfasiri ili aweze kuibaini hadhira ya matini yake 
ya tafsiri ni: je msomaji wa tafsiri yake ni nani? Ana kiwango gani cha 
elimu, ni msomi wa kawaida au msomi aliyebobea? Wana umri gani na ni 
jinsia gani? Je hadhira yake imo katika tabaka gani katika jamii? Baada 
ya kupata majibu ya maswali hayo, mfasiri atakuwa ameibaini hadhira 
yake,na hii itamsaidia mfasiri kuamua umbo la matini yake, kama ataamua 
iwe katika umbo la gazeti, jarida, kijarida, n.k. jambo la kuzingatia 
umbo la matini ya tafsiri ishabihiane na hadhi ya umbo la matini chanzi.
 Kwa kuibaini hadhira ya matini lengwa itamsaidia mfasiri kuamua 
kuirahisisha tafsiri yake au kuifanya iwe ngumu kutegemeana na uwezo wa 
hadhira ya tafsiri lengwa. 
? Unatakiwa kubaini mtindo wa matini chanzi.
Vilevile,
 mfasiri anatakiwa kujua, matini chanzi imetumia mtindo gani katika 
kuwasilisha maudhui yake, imetumia mtindo wa kirasimu? Au imetumia 
mtindo wa kitaaluma? Je imetumia mtindo wa kiuandishi wa habari au 
mtindo wa kimawasiliano yasiyo rasmi? Je ametumia lugha rasmi au ya 
mtaani? Na inatakiwa mtindo wa matini chanzi ilingane na ile ya matini 
lengwa. Tazama mifano ifuatayo: 
Kingereza: Please, Sir do no mind it! If I arrive earlier I’ll wait for you
Kiswahili: Mkubwa! Kausha tu! Na kama nitatia maguu mapema,
 nitakusikilizia Palepale 
Ukiangalia
 mfano huo, utaona kuwa, mitindo iliyotumika katika sentensi hizo ni 
mitindo miwili tofauti, katika mfano tuliouangalia katika lugha chanzi, 
mtindo wa lugha uliotumika ni mtindo rasmi, wakati katika tafsiri [lugha
 lengwa] mtindo uliotumika ni mtindo wa lugha ya mtaani, jambo ambalo si
 zuri katika tafsiri. Mtindo wa lugha lengwa sharti ulingane na mtindo 
wa lugha chanzi. 
hivyo katika mfano huo, mtindo sahihi ungetakiwa kuwa; 
 Tafadhari! usijali! kama nitafika mapema, nitakusubiri. 
? Kusoma matini kwa mara ya mwisho
Jambo
 lingine la kuzingatia ni kuisoma upya matini chanzi. Katika kipengele 
hiki, mfasiri anashauriwa aisome matini chanzi kwa mara ya mwisho huku 
akipigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi 
na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya 
kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au 
kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri 
kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia 
kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri. 
Hayo 
ndiyo mambo ambayo, mfasiri anatakiwa kuyazingatia kabla hajaanza 
mchakato wa kutafsiri. Hivyo basi, sasa tugeukie upande wa pili ambao 
ni: 
 [b] Mambo ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri. 
? Maandalizi ya kutafsiri
Katika
 hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, 
ujumbe wake, mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au 
zisizoeleweka vizuri, anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika 
kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi 
kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina 
maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo 
ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza
 kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri 
au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake. 
? Uchambuzi wa matini chanzi
Katika
 hatua hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, 
nahau, misemo pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika 
au kuyapigia mstari katika hatua ya maandalizi na kuyatafutia visawe 
vyake katika lugha lengwa, hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo 
mbalimbali kama vile, kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na 
istilahi mpya. 
Mfasiri anatakiwa kuwa na shajara au 
daftari dogo kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu
 ya matini chanzi na visawe vyake, visawe vinavyoonekana kufaa 
viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kuvirejelea wakati wa kutafsiri, 
vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini chanzi ni ndefu sana, 
anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo kama vile, 
sura, aya au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya 
nyingine. 
? Uhawilishaji
Uhawilishaji ni 
uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au 
uhamishaji wa mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya 
tafsiri. Hii ina maana kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki 
[kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa katika hatua ya uchambuzi 
huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa]
 na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana 
kwa wasomaji wake. 
? Kusawidi /Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri.
Katika
 hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha 
fulani ya matini aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa
 kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi 
tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi, na hivyo kulazimika 
kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na zaidi marejeo 
yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la kuzingatia, 
mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo na 
lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake. 
? Kudurusu / kuipitia rasimu ya kwanza
Baada
 ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake 
ya tafsiri kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake na 
kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na 
kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la 
na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi. 
? Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu wengine
Baada
 ya mfasiri kuipitia rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa
 makosa yaliyojitokeza, anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu 
hiyo iliyofanyiwa marekebisho ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo 
basi wasomaji hao wanaweza wakahakiki,wakashauri, n.k. Wasomaji hawa 
husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko 
mzuri wenye mantiki. 
? Usawidi /Kuandika rasimu ya mwisho
Baada
 ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia 
maoni, mapendekezo na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake na 
hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho ambayo itakuwa tayari kwa 
kusomwa na wasomaji. 
 Njia / mbinu za Tafsiri
Zipo njia mbalimbali ambazo hutumika katika kutafsiri, baadhi ya njia hizo ni kama vile:
(i) Tafsiri ya neno kwa neno. [Word to word translation]
(ii) Tafsiri sisisi.[ Literal translation]
(iii) Tafsiri ya kimaana/uwazi.[ Semantic translation]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano.[Communicative translation] 
(i) Tafsiri ya neno kwa neno [Word to word translation]
Hii
 ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke 
pweke kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha. Katika 
aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi 
hubakia vilevile bila kubadilika. Na kwa kawaida matini inayotafsiriwa 
huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi. Tazama mifano ifuatayo ya 
tafsiri ya neno kwa neno: 
Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi
Kingereza: He/past/study/until/morning 
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his 
Kiswahili: Anasoma kitabu changu
Kingereza: He/present/book/my 
Kiswahili: Walikula chakula chote
Kingereza: They/past/eat/food/all 
Umuhimu
 wa njia hii, humsaidia mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi 
lugha chanzi inavyofanya kazi, kaina hii ya tafsiri hutumiwa na 
wataalamu wa lugha kuonesha namna maumbo au muundo wa lugha chanzi 
ulivyo, lakini mapungufu yake ni kuwa, aina hii ya tafsiri huwa haitoi 
maana inayokusudiwa kwa uwazi zaidi. 
 
(ii) Tafsiri sisisi [ Literal translation]
Hii
 ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa 
kuzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha
 lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha 
kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo: 
Kingereza: He was taken at the Central Police Station
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.
Badala ya kuwa: Alipelekwa kituo kikuu cha polisi 
(iii) Tafsiri ya kisemantiki/maana au uwazi [Semantic Translation]
Hii
 ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. 
Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi 
jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi hususani vipengele vya 
kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa tafsiri ya 
kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye
 maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi. 
Katika
 aina hii ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo 
lolote unalodhani limekosewa haliruhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo 
marekebisho au ufafanuzi katika tanbihi. Sasa tuangalie baadhi ya mifano
 ya aina hii ya tafsiri: 
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza: He went up to hospital 
 
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: Jane alimwoa John 
Aina
 hii ya tafsiri, ina faida kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa kwa 
kuingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi, mathalani, lugha ya 
Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, 
baadhi ya miundo hiyo ni kama vile: 
Kiswahili: Usiku mwema ? kutoka Kingereza: Good night
Kiswhili: Mabibi na mabwana ? kutoka Kingereza: ladies and gentlemen
Kiswahili: Wako mtiifu ? Kutoka Kiingereza: Yours Sincerel
Kiswahili: Naomba nichukue nafasi hii.. ? Kutoka Kiingereza: May I take this opportunity… 
[Tazama pia Mwansoko na wenzake: 2006] 
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano/ huru [Communicative Translation]
Hii
 ni aina ya tafsiri inayomlenga msomaji [hadhira] wa matini lengwa, 
ambaye katika aina hii ya tafsiri hatarajii kukutana na ugumu wowote 
katika matini atakayoisoma, bali hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi 
ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha yake kwa kadiri 
itakavyoonekana. Hivyo basi, mfasiri wa aina hii ya tafsiri yuko huru 
kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno, methali, 
nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa, pamoja na kuwa tafsiri ya
 kimawasiliano kufuata sarufi ya lugha lengwa ni lazima pia ifuate 
utamaduni, mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa. Tuangalie 
mifano ifuatayo: 
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: John alimwoa Jane 
Kingereza: No need to cry over spilt milk
Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki 
Kiingereza: What comes around goes arround
Kiswahili: Mla vya watu, naye vyake huliwa. 
Kiswahili: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
Kiingereza: A friend in need is a friend in need 
Kiswahili: Bahati haiji mara mbili
Kiingereza: Golden chance never comes twice 
Aina
 hii ya tafsiri hulenga kutoa athari ile ile au inayokaribiana kwa 
hadhira ya matini lengwa kama ilivyo kwa hadhira ya matini chanzi[ 
matini asilia], hii ni aina ya tafsiri ambayo hutumika sana kufasiri 
mawazo ya kigeni katika lugha na mazingira mapya, mawazo ambayo huelezwa
 katika misingi ya lugha, utamaduni na mazingira yanayoeleweka kwa 
hadhira ya matini lengwa.  
Ebu tuangalie baadhi ya 
mifano tuliyoiangalia katika tafsiri ya Kisemantiki [maana] tunavyoweza 
kutafsiri katika njia ya tafsiri ya kimawasiliano:
Kiingereza Kiswahili
Good night Lala salama
Ladies and Gentlemen Ndugu zangu
Yours Sincerely Ni mimi
May I take this opportunity to… Naomba mnisikilize 
Hivyo
 basi, katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo 
inayopatikana katika lugha lengwa inayohusiana au kukaribiana na ile ya 
lugha chanzi. Ebu jaribu kutafsiri misemo/methali zifuatayo ya lugha ya 
Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza: 
Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
Asiyekubali kushindwa si mshindani
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa
Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Dua la kuku halimpati mwewe
Bandubandu humaliza gogo
Jogoo wa shamba hawiki mjini
La kuvunda halina ubani
Mtegemea cha nduguye hufa masikini 
 
Faida
 ya aina hii ya tafsiri, humfanya mfasiri kuwa huru kutumia maneno au 
mafungu ya maneno ambayo huweza kutoa athari ile ile au inayokaribiana 
na maneno au mafungu ya maneno katika matini ya lugha chanzi, lakini 
mapungufu ya aina hii ya tafsiri huweza kutokea iwapo mfasiri ataamua 
kuegemea mno kwenye mawazo, historia, mazingira au itikadi ya lugha 
lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo: 
Kingereza: The Merchant of Venice
Kiswahili: Mabepari wa Venisi 
Ukiangalia
 mfano huo utaona kuwa, The Merchant of Venice, tamthiliya iliyoandikwa 
na William Shakespeare, ingefaa pia kufasiriwa kuwa, Wafanyabiashara wa 
Venisi, lakini Mwalimu J.K Nyerere aliamua kuifasiri kuwa, Mabepari wa 
Venisi kutokana na kuwa Nyerere ndiye mwasisi wa itikadi ya Ujamaa 
nchini Tanzania, hivyo aliegemea katika itikadi kufasiri. 
Hivyo
 basi, mtu anapokuwa anafanya kazi ya kufasiri, maandishi yo yote kutoka
 lugha moja kwenda lugha nyingine atajikuta akiangukia katika moja wapo 
ya njia tulizozijadili hapo juu, lakini ikumbukwe tafsiri ya neno kwa 
neno ni nadra sana kutumiwa na wafasiri wengi, na njia hizo huweza 
kuingiliana katika matini moja ya tafsiri. 
 
 
 
Ukalimani [Interpritation]
Ukalimani ni nini?
Ukalimani
 imefasiliwa kuwa ni, uhusishaji wa kuhamisha maana kutoka lugha moja 
(lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa) katika mazungumzo. 
Hivyo basi tunaweza kusema pia, ukalimani ni hali ya mtu kuhamisha 
mawazo ya kinachozungumzwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine 
katika mazungumzo. Hii ina maana kuwa ukalimani ni lazima uhusishe pande
 mbili, upande wa kwanza sharti awepo mtu anayezungumza lugha fulani na 
upande mwingine kunakuwa na mtu ambaye anasikiliza hicho 
kinachozungumzwa na kuyarudia hayo yanayozungumzwa kwa kutumia lugha 
nyingine tofauti na ile iliyotumiwa na mazungumzaji wa kwanza.
Hivyo
 basi, ukiangalia, maana hiyo tuliyoiangalia utaona kuwa, ukalimani ni 
taaluma inayohusu mazungumzo wakati tafsiri yenyewe uhusu maanadishi, 
kwa maana hiyo huwa tunatafsiri maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha
 nyingine na tunakalimani mazungumzo kutoka lugha moja kwenda lugha 
nyingine.
Ukalimani ulianza pale ambapo mataifa mbalimbali yenye 
kuzungumza lugha tofauti tofauti yalipoanza kuingiliana na kushirikiana 
katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa, kichumi na kiutamaduni, 
kwa mfano ujio wa wageni Afrika Mashariki kama vile Waarabu, Wajerumani 
na Waingereza ili waweze kuwasiliana na wenyeji wao waliambatana na watu
 ambao walikuwa wakiwatumia kama wakilamani wao.
Kwa sasa hivi 
ukalimani umekuwa kama taaluma muhimu, ukalimani unafanyika katika 
mahakama, kanisani, katika mikutano ya kimataifa, mahubiri ya kidini, 
n.k na kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna vifaa 
maalumu ambayo hutumika kukalimani mazungunzo kutoka lugha moja kwenda 
lugha nyingine, ambayo huvaliwa masikioni katika kumbi za mikutano. Na 
sasa ni taaluma inayofundishwa katika shule za sekondari na elimu ya juu
 kama ilivyo kwa tafsiri kutokana na umuhimu wake.
Mkalimani ni 
mtu muhumi sana katika kufanikisha mawasiliano kwa watu wanaotumia lugha
 mbili tofauti, au lugha inayotumika katika eneo hilo msikilizaji 
haielewi na haijui na ndiyo maana utakuta wakalimani wakihitajika 
mahakamni, mikutano ya kimataifa, katika mahubiri ya kidini au mahali 
popote pale ambapo wazungumzaji hawawezi kuelewana kwa kuwa wanatumia 
lugha tofauti.
Sifa za mkalimani bora
? Awe mtu anayezielewa lugha chanzi na lugha lengwa vizuri
? Awe ni mtu ambaye ameishi pande zote za lugha anazozikalimani ili kuelewa mila na desturi za watumiaji wa lugha hizo.
?
 Awe stadi wa ukalimani, hapa inatakiwa awe na uhodari wa kukalimani, 
kuzungumza vizuri, maneno kusikika, awe na uwezo wa kukalimani neno kwa 
neno au sentensi na sentensi, kutumia ishara zinazoambatana na ishara za
 mzungumzaji wa lugha chanzi na hata kutumia mtindo anaodhani unaweza 
kuwavutia wasikilizaji wake.
? Muadirifu, ambaye hawezi kupotosha
 au kubadili ukweli wa kinachozungumzwa, nah ii ni muhimu kwa sababu 
wakalimani hutumika hadi mahakami hivyo kama si mwadirifu huweza 
kuufanya upande mmoja ukakosa haki inayostahiri.
? Asiwe mbaguzi,
 hapa ina maana mkalimani asiamue kupotosha ukweli wa kile 
kinachozungumzwa kwa kuwa tu kinaendana kinyume na itikadi yake ya 
kisiasa, kidini, kiutamaduni, n.k. wala asiangalie jinsia ya mtu umri au
 hali ya mtu anayemfanyia ukalimani.
 Mambo ya kuzingatia katika Ukalimani
Kwa
 ujumla yapo mambo kadha wa kadha, ambayo mkalimani anatakiwa 
kuyazingatia anapotaka kufanya ukalimani, mambo hayo tunaweza kuyagawa 
katika makundi mawili, ambayo ni:
1. Kabla ya kuanza ukalimani
Katika hatua hii, mkalimani anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a)
 Awe na uelewa mzuri wa lugha zote anazotaka kukalimani, hapa tuna maana
 kuwa awe na uwezo wa kuzungumza na kuelewa lugha chanzi na lugha lengw,
 hii itasaidia mkalimani kutopotosha kile kinachozungumzwa na 
mzungumzaji wa lugha chanzi.
(b) Awe anaijua historia na utamaduni wa jamii zote mbili, yaani ile ya lugha chanzi na ile ya lugha lengwa.
(c)
 Kama ni ukalimani rasmi, ni vizuri kwa mkalimani akamjua mzungumzaji wa
 lugha chanzi, ni vema pia ukafanya naye mazungumzo kidogo ili kumzoea, 
na kutambua vionjo vyake ili iwe rahisi kwa mkalimani pindi atakapokuwa 
anafanya ukalimani asionekane kama mgeni.
(d) Vilevile ni muhimu 
kwa mtu anayekalimani, akawa na uelewa mzuri wa mada inayozungumzwa, hii
 itamrahisishia mkalimani katika ukalimani wake.
2. Katika ukalimani wenyewe
Mkalamani
 anapokuwa amesimama mbele ya hadhira [wasikilizaji] pamoja na 
mzungumzaji wa lugha chanzi kwa ajili ya kuanza ukalimani, anatakiwa 
kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Kuwa makini katika kusikiliza 
kile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ili kuepuka kuachwa
 mahali na kuepuka kumuomba mzungumzaji kurudia mara kwa mara.
(b)
 Itambue hadhira ya lugha lengwa, ni watu wa namna gani, wana kiwango 
gani cha elimu, ni wasomi wa kawaida au waliobobea, ni watu wa jinsia na
 umri gani,? Hii itakusaidi kujua aina ya msamiati na miundo ya tungo 
utakayoitumia, kama iwe rahisi au migumu kutokana na hadhira yako 
ilivyo.
(c) Tumia mitindo unayodhani itaeleweka vema na hadhira/ 
wasikilizaji wa lugha lengwa, kwa mfano kama hadhira yako ni vijana, 
jaribu kutumia mitindo inayopendwa na vijana, kama wasikilizaji wako ni 
watu rasmi na we huna budi kuwa rasmi.
(d) Weka mkazo sehemu 
ambazo mzungumzaji wa lugha chanzi anaweka mkazo ili kuepuka utofauti 
yako na mzungumzaji wa lugha chanzi, na hata kuepuka kuathiri lengo la 
mzungumzaji wa lugha chanzi.
(e) Unatakiwa pia kutumia ishara 
zinazotumiwa na mzungumzaji wa lugha chanzi, hii itawafanya wasikilizaji
 waamini kile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ndiyo 
kilekile kinachozungumzwa na mkalimani.
(f) Usiwe muda mwingi 
unamtazama mzungumzaji wa lugha chanzi na kusahahu kuitazama hadhira 
yako, hivyo unatakiwa kuitazama hadhira yako ili kugundua kama wako 
pamoja na wewe au kuna sehemu hawajakuelewa ili uweze kuwafafanulia 
zaidi.
(g) Muombe mzungumzaji wa lugha chanzi kurudia sehemu 
unayodhani hujaisikia au hujaielewa vizuri, kwani ni makosa kwa 
mkalimani kukalimani sehemu au jambo ambalo hukulisikia vizuri au 
kulielewa.
Hivyo basi hayo ndiyo mambo muhimu ambayo mkalimani 
anatakiwa kuyazingatia anapokuwa anafanya ukalimani. Jambo la 
kuzingatia, mkalimani hutakiwa kuingiza hisia zako unapokuwa anafanya 
ukalimani. na ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango ambacho mila na 
desturi zote yaani za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana ama 
kushabihiana.
 Dhima za Tafsiri na Ukalimani
Tafsiri na Ukalimani ina dhima zifuatazo:
? Hutuwezesha kujifunza lugha tofauti.
Kati
 ya mazoezi mazuri anayoweza kutumia mtu katika kujifunza lugha 
nyingine, basi zoezi la kutafsiri au kukalimani mara kwa mara humsaidia 
mtu kujifunza lugha kwa urahisi zaidi, kwani kwa kufanya tafsiri ya mara
 kwa mara kutamsaidia mtu kugundua miundo na vipengele mbalimbali vya 
lugha na jinsi vinavyofanya kazi katika lugha anayojifunza. 
? Hutumika kama njia ya mawasiliano.
Kutokana
 na maingiliano ya mataifa mbalimbali yanayotumia lugha tofauti tofauti,
 tafsiri hutumika kurahisisha mawasiliano baina ya makundi ya watu 
wanaotumia lugha tofauti tofauti, hutumika kutolea maelezo ya kibiashara
 kama vile maelekezo ya jinsi ya kutumia bidhaa mbalimbali 
zinazozalishwa nje au zinazouzwa nje ya nchi, katika matangazo ya 
kitalii ili kuwavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali, vilevile 
hutumika katika vyombo vya habari, tafsiri pia inatumika katika nyaraka 
rasmi, mikataba, vitabu vya ziada na kiada, lakini pia ukalimani 
hulahisisha mawasiliano miongoni mwa watu wanaozungumza lugha tofauti. 
? Tafsiri na Ukalimani hutumika kueneza utamaduni.
Tafsiri
 imekutanisha lugha na tamaduni mbalimbali duniani na kusababisha 
tamaduni na lugha hizo kuathiriana, kwa mfano mara baada ya waarabu 
kuingia Afrika Mashariki na vitabu mbalimbali vya Kiarabu na Kiislamu 
kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ilisababisha utamaduni wa Kiswahili 
kuathiriwa na utamaduni wa Kiarabu na Kiislamu kutoka na kuiga kwa mambo
 mengi kutoka huko, lakini pia hata walipokuja wazungu na kutafsiri 
vitabu vyao vya kifasihi, kutafsiriwa kwa Biblia, n.k. ilisababisha pia 
utamaduni wa Mswahili kuathiriwa na utamaduni wa Ulaya. 
? Tafsiri na Ukalimani ina dhima ya kuwasilisha ujumbe wa manufaa kwa watu ambao hawafahamu lugha chanzi [lugha asilia] 
 Changamoto/ mapungufu katika tafsiri na Ukalimani
Mfasiri
 katika kazi yake ya kufasiri hukumbana na changamoto mbalimbali, ambazo
 huweza kusababisha tafsiri kuwa na mapungufu ya hapa na pale. Baadhi ya
 changamoto au mapungufu hayo ni kama vile: 
(i) Tofauti za kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.
Tofautui
 za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya 
Kingereza wakati mwingine husababisha matatizo au upungufu katika 
tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo ya vitenzi vya Kiingereza 
huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au wingi wa wahusika wala
 majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa 
tofauti maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na wingi 
wa wahusika na hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano 
ifuatayo kama ilivyotolewa na, Mwansoko [2006] 
Kingereza Kiswahili
No parking ? Usiegeshe gari hapa [je kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]
No Smoking ? Usivute sigara[ Je ni sigara tundiyo hairuhusiwi kuvutwa?]
Arrivals ? Wanaowasili
Departures ? Wanaosafiri 
Vilevile tofauti za maana kati ya lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani, mathalani: 
Kiswahili Kingereza
Wasiojiweza ? Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni walemavu]
 [na siyo walimavu wote hawajiwezi]
Wezi wa mifukoni? Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka mifukoni] 
(ii) Tofauti za mitindo kati lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
 za mitindo ya uzungumzaji pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na 
hii ni kwa sababu unaweza kukuta kuna mitindo fulani inaweza kutumika 
katika muktadha fulani lakini ikishindwa kupata tafsiri katika lugha 
nyingine katika muktadha ule ule.mathalani: 
 Kingereza: Kiswahili 
(i) Thou shalt not steal [mtindo wa kidini] ? Usiibe 
 Do not steal [mtindo wa kawaida] ? Usiibe 
(ii) Lend me your ears [mtindo wa kishairi] ? Naomba mnisikilize
May I have your attention [kawaida] ? Naomba mnisikilize 
Tafsiri
 zote tulizoziangalia katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au 
taarifa ili ile iliyomo katika matini chanzi lakini tafsiri hizo 
hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika katika matini chanzi. 
(iii) Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
 za kiutamaduni, yaani taofauti za kimila, desturi na mazingira ya 
watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufanya tafsiri au 
ukalimani kuwa mgumu, kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza wana 
milo minne wakati Waswahili wana milo mitatu na hii hupelekea kuwa 
vigumu kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika dhana ya 
Kiswahili. Mfano: 
Waingereza wana: Waswahili wana:
 Breakfast ------------------ Kifungua kinywa
 Lunch …………………... Chakula cha mchana
 High tea ……………………?
 Dinner ……………………Chakula cha jioni
 Supper …………………….? 
Kwa
 hiyo ukiangalia mifano hiyo, utaona kuwa, high tea na supper kuzipata 
dhana zake katika lugha ya Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na 
utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu 
kupata tafsiri ya vyakula kama vile ugali, makande katika lugha ya 
Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya aina hiyo. 
(iv) Tofauti za kiitikadi kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti
 za kiitikadi pia huweza kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwa 
sababu, utakuta wafasiri wengi hususani waandishi wa habari kuegemea 
katika itikadi zaidi, kwa mfano: 
Kingereza Kiswahili
Bussnessman ? mlanguzi [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi
 ya ujamaa] 
 mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na 
 itikadi ya ubepari] 
Freedom fighter ? wapigania uhuru [Tafsiri ya vyombo vya habari vya 
 Tanzania wakati wa kupigania uhuru] 
 Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika
 Kusini wakati huo]
Hivyo
 basi kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, ukalimani mzuri unawezekana 
kwa kiwango ambacho mila na desturi zote yaana za lugha chanzi na lugha 
lengwa zinalingana ama kushabihiana.
Na kutokana na umuhimu wa 
taaluma hii ya tafsiri na ukalimani, serikali kupitia Baraza la 
Kiswahili la Taifa Bakita [BAKITA] imeanzisha idara maalumu ya Tafsiri 
na Ukalimani, na idara hiyo ina majukumu yafuatayo:
? Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mbalimbali kwa masharika, idara, wizara, balozi na watu binafsi.
?
 Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye mikutano ya kitaifa na 
kimataifa na katika shughuli za masharika, makampuni na watu binafsi.
? Kupitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na asasi mbalimbali au wafasiri wa nje.
? Kutoa ushauri kuhusu masula ya tafsiri na ukalimani.  
 MAZOEZI
? Zoezi la kwanza
Fasili matini ifuatayo kwenda lugha ya Kiingereza:
 MTO
(Siku ifuatayo, asubuhi. Ngoswe na Mitomingi wako kazini. Wanafika nyumba moja).
MITOMINGI: Hodi! Hodi! Wenyewe! (Kimya, hakuna sauti itokayo). Hodi wenyewe
 (Kimya) Labda hawajaamka.
NGOSWE: Kama bado wamelala tuwaache kwanza tuwarudie baadaye.
MITOMINGI: Mimi naona itakuwa shida shida kwani nyumba za hapa zimesambaa
 mno.hebu nibishe tena.hodi! hodi! Wenyewe mpo?(Akinyamaza na
 kunapita kimya. Punde mlango wafunguka na kipande cha
 mwanamke chatokeza). Habari za asubuhi mama? 
MAMA: Salama, mwaonaje?
MITOMINGI
NGOSWE Hatujambo
MAMA: Sijui niwasaidie nini akina baba?
MITOMINGI: Mwenyewe yupo sijui?
MAMA: (Akitazama chini mwenye huzuni anatingisha kichwa). Hayupo
MITOMINGI: Katoka kitambo?
MAMA: (Akimtazama Mitomingi kwa jicho kali). Ni marehemu.
MITOMINGI: (Amtazama Ngoswe ambaye kainamisha kichwa na wote wanamtazama
 kwa jicho la huruma). Pole mama.
NGOSWE: Pole mama.
MAMA: Nimekwisha poa.
MITOMINGI: Samahani mama , hata sikufahamu.
MAMA: Sio neno baba sio kosa lako.
MITOMINGI: Mungu mkubwa.
MAMA: Nifanyeje; kazi ya Mungu haina dosari. (Ananyamaza kwa kitambo). Je
 niwasaidie nini?
MITOMINGI: Jambo moja dogo tu. Samahani kama nitakusumbua maana kwanza ni
 asubuhi tena yenyewe ni msiba,
MAMA: Sio kitu baba.
MITOMINGI: Nadhani umepata kumsikia Balozi Mitomingi.
MAMA: Nimemsikia lakini kumwona bado.
MITOMINGI: Basi mama, huyo Mitomingi, Ngengemkeni Mitomingi ndiye mimi.
MAMA: (Kwa mshangao): Karibuni ndani mpumzike
MITOMINGI: Hatukai sana mama.
MAMA: Basi ngoja niwatolee viti make. (Aingia ndani na kutoka na viti viwili
 kuwapatia wageni. Yeye aketi chini).
MITOMINGI: Mama!
MAMA: Baba!
MITOMINGI: Nadhani una habari juu ya kuhesabu watu.
MAMA: (Kwa mshangao): Kuhesabu watu?
MITOMINGI: Ndiyo kuhesabu watu.
MAMA: Kuhesabu watu! (Akitingisha kichwa) Hapana.
MITOMINGI: Balozi wenu hakuwajulisha?
MAMA: Hata kidogo.
MITOMINGI: Kweli?
MAMA: Kwani Tambitambi naye mtu yule!
 Pombe na yeye ni pete na chanda!
 Hajali Balozi wake wala nyumba yake.
MITOMINGI: Ni sawa usemayo mama. Tambitambi yule akili hazimtoshi. Tumefika
 kwake wala hajulikani aliko!
MAMA: Kama kuna wanaume mabwege yule ametia for a.
MITOMINGI: Usizidi kunambia mama, Tambitambi mambo yake hakuna
 asiyeyafahamu…. Sasa mama!....
MAMA: Ndiyo baba.
MTOMINGI: Sisi kama utuonavyo tuko shughulini, shughuli hiyo si nyingine bali hiyo
 niliyoisema sasa hivi kuhesabu watu. Na huyu kijana ndiye karani
 mwenyewe ahusikaye. Ingekuwa bora kama wewe na wanao wote
 mngetoka nje ili tufanye kazi yetu.
MAMA: Sasa baba mbona itakuwa vigumu.
MITOMINGI: Kwa vipi?
MAMA: Sasa baba utahesabu vipi?
MITOMINGI: Kwa nini?
MAMA: Kama utatuhesabu wewe basi u mchawi.
MITOMINGI: Mbona sikuelewi!
MAMA: Mchawi ndiye anayehesabu watoto wa wenzake ili awaroge. Sasa wewe
 umchawi? Hata kama u mchawi siwezi kukubali utuhesabui maana
 siwezi kujua nia yako ni mbaya au nzuri.
MITOMINGI: Mtu akuwaniae uovu haji kweupe.
MAMA: Sawa usemayo baba.
NGOSWE: Sasa mama hebu walete wanao na yeyote yule aliye ndani.
MAMA: Wanangu hawapo wamekwenda shamba kuwania mpunga.
NGOSWE: Wote?
MAMA: Ndiyo.
NGOSWE: Ndio kusema hakuna kiumbe hata kimoja?
MAMA; Yuko mke mwenzangu.
NGOSWE; Tuitie.(Mama anasimama kwa unyonge na kuingia ndani. Anarudi peke
 yake baada ya muda mfupi). Yu wapi?
MAMA: Aja (Punde mama mwingine atokea. Yu kariby rika moja na mama wa
 kwanza isipokuwa huyu mbichimbichi).
MITOMINGI: Habari mama?
NGOSWE: (Wakati huohuo) Shikamoo.
MAMA WA PILI: Nzuri (Atazama chini kwa aibu huku akiketi).
NGOSWE: (Akimtazama mama wa kwanza). Basi; hakuna mtu mwingine ndani?
MAMA WA PILI: (Akikataa kwa kichwa)
MITOMINGI: (Kwa mama wa kwanza). Lakini nyie wanawake mbona waoga sana!
 Hivyo mnataka kuniambia motto wa mgongoni anaweza kwenda
 kuwania mpunga? (Mama agutuka). Hebu niambie mwanao mchanga
 yu wapi?
MAMA WA KWANZA: Sina mtoto mchanga. 
 
MITOMINGI: Hivyo mama wasema kweli?
MAMA WA KWANZA: Haki vile.(Mara kwasikika sauti ya mtoto akilia ndani ya 
 nyumba). 
MITOMINGI: Na huyo anayelia kama si mtoto ni nini/ (Mama ainuka wakawaka na
 kuingia ndani kwa aibu. Muda wapiti na harudi). Mama! Njoo basi
 tumalize shughuli. Usijali mambo ya motto kulia, ni jambo la kawaida.
 (Mama atokea amepakata mtoto mchanga. Aketi chini na sasa uso wake
 umejaa hasira na chuki)…
 [Imenukuliwa kutoka, Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. Uk 13-15]
? Zoezi la pili
1. Linganisha na linganua kati ya taaluma ya tafsiri na ukalimani. 
 2. (a) Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiingereza
(i) Dua la kuku halimpati mwewe
(ii) Bandu bandu humaliza gogo
(iii) La kuvunda halina ubani
(iv) Mla vya watu naye vyake huliwa
(v) Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwa nini? 
??Zoezi la tatu 
1. [a] Kwa kutumia mifano, fafanua istilahi zifuatazo:
 [i] Matini chanzi
 [ii] Matini lengwa
 [iii] Lugha chanzi
 [iv] Lugha lengwa 
 
[b] Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiswahili
(i) All that glister is not gold
(ii) Looser casn't be a chooser
(iii) When you make your bed you must lie on it
(iv) There is no incense for something rotting
(v) When in Rome do, do as Romans do
(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri hizo ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwanini?
2. "Mfasiri au mkalimani hukabiliana na changamoto mbalimbali katika kufanikisha kazi
 yake." Huku ukitumia mifano thibitisha kauli hiyo. 
 MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
 Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam 
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press 
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
 Oxford University Press Dar-es-salaam 
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
 D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam 
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. 
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2011 
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2011 
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2011 
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
 Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman
AN ONLINE PLATFORM THAT PROVIDES EDUCATIONAL CONTENT,SYLLABUSES, STUDY NOTES/ MATERIALS ,PAST PAPERS, QUESTIONS & ANSWERS FOR THE STUDENTS,FORM I--VI ,RESITTERS,QT, ADULT LEARNERS, COLLEGE STUDENTS, PUPILS, TEACHERS, PARENTS,TEACHERS OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA AND WORLDWIDE.YOU ARE WELCOME TO SHARE YOUR KNOWLEDGE AND IDEAS.ENJOY MASATU BLOG.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE. "LEARN.REVISE.DISCUSS".Anytime, Anywhere.
- HOME
- UTAKUZAJE UWEZO WAKO WA LUGHA ?
- MBINU ZA KUSOMA NA KUFAULU MITIHANI
- HOW TO IMPROVE YOUR MEMORY
- ONLINE LEARNING & DISTANCE LEARNING ( E--LEA...
- O-LEVEL & A--LEVEL SYLLABUS
- FORM FOUR ( F 4 )--SUBJECTS---TANZANIA
- FORM TWO ( F 2 )--SUBJECTS---TANZANIA
- FORM ONE ( F 1 )-- SUBJECTS---TANZANIA
- FORM FIVE( F 5 ) AND SIX ( F 6 )--SUBJECTS ---TANZANIA
- FORM THREE ( F 3 ) SUBJECTS----TANZANIA
- STANDARD 1 & 2 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA 1 & 2-...
- STANDARD 3 & 4 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA 3 & 4...
- STANDARD 5, 6 & 7 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA...
 
 
No comments:
Post a Comment