FASIHI SIMULIZI VIPERA NA TANZU ZAKE.
Kwa
mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni
kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi
karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi
zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia
kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi. Kwa upande wa
nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni
kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa
upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi
Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari
kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987)
Mulika
namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na
wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili
lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu
tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.
Hivyo
basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za
Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo
mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa
vinavyotumika na namna ya uimbaji.
Fasihisi
Simulizi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni
M.M.Mulokozi (1996) anasema Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa
kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia
maandishi.
TUKI
(2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka
kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na
vitendawili.
Hivyo
basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa,
hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.
Tanzu
ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za
kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano,
tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi
(Wamitila (2003).
Vipera
ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi.
Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)
M.M.Mulokozi
katika makala yake ya tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba
21(1989) amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo
viwili ambavyo ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na
kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.
Umbile
na tabia ya kazi inayohusika: katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele
vya ndani vinavyoiumba sanaa hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya
vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari,
kimafumbo, kiwimbo na kighani), muundo wa fani hiyo na wahusika.
Kwa
upande wa muktadha na namna ya uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi
ni tukio hivyo huambatana na muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha,
watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio
unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa
hadhira, kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo,
utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea
muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).
Kwa
hiyo kwa kutumia vigezo hivi, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi
Simulizi kama ifuatavyo;
Masimulizi;
hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa
utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha
inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha
muundo, mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu
nyingine kama vile ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa
moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni
kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili
ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya
uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira.
Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya
mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum. Mfano,
baada ya kazi.
Masimulizi
yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni)
na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja
ambacho ni ngano. Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo
wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni
kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea
au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo
cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha
vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.
Istiara;
hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine
iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha
ambayo ni lugha ya mafumbo.
Mbazi;
hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi
au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha
dhima.
Kisa;
hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika
ni kigezo cha kidhima.
Utanzu
mwingine wa masimulizi ni utanzu wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera
vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
Visakale;
haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye
kuchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika
hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani.
Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.
Mapisi;
haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo
kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo
ya kweli.
Tarihi;
haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo
kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na
tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa
kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.
Kumbukumbu;
haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu.
Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo
kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.
Visasili;
hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi
ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika
kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha
kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.
Utanzu
mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa Semi. Semi ni tungo au kauli fupi fupi
za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa
utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni
kigezo cha kidhima ambacho ni kufunza.
Utanzu
huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili,
misimu, mafumbo na lakabu.
Methali
ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito
yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni
kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha
muundo ambapo methali huundwa na muundo wa pande mbili ambazo hutegemeana.
Vitendawili;
huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo
vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya
kimafumbo.
Misimu;
ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira
maalum. Hivyo vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha
yaani hutokea wakati maalum na mazingira maalum.
Mafumbo;
ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo
kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha
lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.
Lakabu;
haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na
sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika
katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha
kificho yaani maana yake hufichwa.
Utanzu
mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi
unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa
kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha
ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani
inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.
Katika
utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;
Nyimbo
ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni
kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji,
muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha
muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na
wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu
wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea,
kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za
vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.
Tumbuizo;
hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali
kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho
hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo
huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.
Bembea;
hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha
kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.
Kongozi;
hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima
ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake
ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.
Nyimbo
za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu.
Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu
au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha
wa kidini.
Wawe;
hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo
huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake
ni kuchapusha kazi.
Tenzi;
hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo
cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.
Tendi;
hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo
vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye
historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha
yake ni ya kinathari.
Mbolezi;
hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa
maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima
yake ni kuomboleza.
Kimai;
hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni
kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo
cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.
Nyiso;
hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo
kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira
maalumu, kama vile porini nakadhalika.
Nyimbo
za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo
muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika
au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.
Nyimbo
za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo
vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa
michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo
waimbaji wake huwa ni watoto.
Nyimbo
za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa
shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au
waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha
ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.
Nyimbo
za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa
ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.
Nyimbo
za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile,
kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo
vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa
kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.
Maghani;
hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa
mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya
ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo
vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.
Kipera
hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani
masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani
mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa,
maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.
Sifo;
hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo
huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni
kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo
kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na
tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.
Kivugo;
hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha
zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina.
Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu
pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio
maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha
uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea
shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa
papo kwa papo.
Tondozi;
hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi
ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa
kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama
ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.
Ghani
masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au
tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha
lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani
iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha
namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.
Ghani
masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.
Rara
ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha
inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani
ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo
kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na
ala za muziki.
Ngano;
hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika
kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni
muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano
huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.
Sifo;
hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo
huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha
iliyotumika ni lugha ya kishairi.
Tendi;
hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito
kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani
ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni
muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.
Utanzu
mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongozi au
maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila
mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina
fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha
ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha
kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia.
Utanzu
huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani,
soga, mawaidha na ulumbi.
Hotuba;
haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa
au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha
ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo
cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano
katika vikao rasmi au mikutano.
Malumbano
ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao
wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na
wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha
ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo
wahusika huwa na uhusiano wa karibu.
Soga;
haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake
ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha
inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake
huwa ni mahali popote.
Mawaidha;
haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo.
Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo
dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.
Ulumbi;
huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo
vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha
iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.
Utanzu
mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo
hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili
kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika
kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa
kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni
kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo
maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe
fulani na katika matukio ya kijamii.
Utanzu
mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya
kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu
huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine
ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii.
Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.
Pamoja
na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi
kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa
tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-
Vigezo
vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha
huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.
Pia
kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi
mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo.
Vilevile
kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na
mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na
kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo.
Kwa
kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi
Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani,
kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji
wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo
katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi
tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.
MAREJEO:
Mulokozi,
M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi:
Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.
Mulokozi,
M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi
Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.
Wamitila,
K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi
na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.
TUKI,
(2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu.
(Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).