Kufanyia
 kazi zako nyumbani, iwe umeajiriwa au umejiajiri au  wewe  ni  
mwanafunzi wa  shule  za   msingi , sekondari  au  chuo   kuna faida 
nyingi sana, baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;
- Unaokoa muda mwingi ambao huwa unaupoteza kwa kwenda eneo la kazi, shule au chuo Kuanzia muda unaotumia kwenda, kurudi na mwingine unaopotea, kwa kufanyia kazi nyumbani hupotezi muda wako.
- Unapunguza fursa za kupoteza muda zinazopatikana kwenye eneo la kazi, mfano mikutano mbalimbali ambayo hufanyika maeneo ya kazi, ambayo kwa sehemu kubwa haina tija.
- Unafanya kazi kwa mpango wako bila ya kusumbuliwa na wafanyakazi wengine.Kama mwanafunzi au mwanachuo unaepuka kelele za wanafunzi wenzako . Japo kunakuwa na mawasiliano ya simu au njia nyingine za mtandao, ile hali ya kukatishwa na wengine wakati unafanya kazi au unajisomea inapungua.
- Kwa sehemu kubwa unakuwa na uhuru wa kupanga muda wako mwenyewe, hasa kama kazi yako haihitaji kushirikiana na wengine wakati mnaifanya. Unaweza kupanga kufanya kwa muda unaofaa kwako.
- Unapata muda mwingi wa kupumzika, majukumu yako unayofanya ukiwa kazini, shule , chuo ukiyafanyia nyumbani itakuchukua nusu ya muda unaotumia kuyafanya ukiwa kazini , shule au chuo .Hivyo unapata muda mwingi wa kupumzika au kufanya mambo mengine.
Changamoto za kufanyia kazi nyumbani.
Hakuna kisichokuwa na changamoto, na katika kufanyia kazi nyumbani, zipo changamoto nyingi. Hapa ni baadhi ya changamoto hizo;
- Kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa wakati kwa sababu hakuna anayekusimamia moja kwa moja au anayekuangalia. Unahitaji nidhamu kali sana kuweza kujisimamia mwenyewe.
- Usumbufu wa wanafamilia wakati unafanya kazi, wengi hawajui kwamba japo upo nyumbani pia upo kazini, hivyo kuingilia kazi zako pale wanapokuwa na mahitaji mbalimbali.
- Kukosekana kwa mipaka kati ya kazi na maisha. Kwa kuwa unafanyia vyote nyumbani, ni rahisi kushindwa kuweka mipaka, ukajikuta unaruhusu mambo ya kifamilia kuingia kwenye wakati wa kazi au mambo ya kikazi kuingia kwenye wakati wa familia.
- Wageni usiokuwa na miadi nao wanapokuja nyumbani na kujua upo, wanaingilia sana muda wako wa kazi. Wengi hawawezi kuelewa kwamba japokuwa upo nyumbani, upo kazini, hivyo kuhitaji muda wako mwingi.
- Ni rahisi kwa uvivu kukunyemelea, ukipatwa na usingizi kidogo ni rahisi kwenda kulala au kufanya mambo mengine ya kupoteza muda kama kuangalia tv, kuzurura mitandaoni na kadhalika.
MKAKATI  BORA  KWAKO  WA   KUFANYIA  KAZI  NYUMBANI.
Ili
 kupata manufaa ya kufanyia kazi nyumbani, pamoja na kuzuia changamoto 
zake zisiwe kikwazo kwako, tengeneza mkakati mzuri kwako kufanyia kazi 
nyumbani
Zingatia mambo yafuatayo katika kutengeneza mkakati wako wa kufanyia kazi nyumbani utakaokupa matokeo mazuri.
( 01 ). TENGA  ENEO  LA  KUFANYIA  KAZI.
Kitu
 cha kwanza muhimu kabisa kwako kufanya ni kutenga eneo la kufanyia kazi
 ukiwa nyumbani. Huwezi kuwa unafanyia kazi kila mahali na ukawa na 
nidhamu nzuri. Badala yake unapaswa kutenga eneo ambalo utakuwa 
unafanyia kazi zako, na ukiwa eneo hilo unachofanya ni kazi tu na siyo 
kitu kingine.
Hii
 inakuandaa kisaikolojia kuheshimu eneo hilo na unapokuwa kwenye eneo 
hilo unajua cha kufanya ni kazi. Kama unaishi kwenye nyumba kubwa 
unaweza kutenga chumba utakachotumia kama ofisi. Lakini kama huwezi 
kufanya hivyo unaweza kutenga eneo kwenye chumba chochote, hata kile 
unacholala na kulitumia kama eneo la kazi.
Kama
 unatenga eneo ndani ya chumba chenye matumizi mengine, hakikisha 
unaweka kiti na meza kwa ajili ya kufanyia kazi. Hivyo unapokaa kwenye 
kiti na meza hiyo, unajua kabisa hili ni eneo la kazi. Usifanye kitu 
kingine unapokuwa kwenye kiti na meza ulivyoandaa kwa ajili ya kazi.
Epuka
 kufanyia kazi kitandani au kwenye kochi, kwenye maeneo hayo hutaipa 
kazi uzito kwa sababu kisaikolojia unayachukulia kama maeneo ya 
kupumzika
 ( 02 ). TENGENEZA  RATIBA  YAKO  YA  KILA  SIKU  NA  IFUATE.
Japokuwa
 una uhuru wa muda gani ufanye kazi unapokuwa nyumbani, uhuru huo una 
mipaka. Huwezi kufanya kazi zako pale unapojisikia, ukienda kwa mpango 
huo hutafanya chochote. Ndiyo una uhuru, lakini lazima utengeneze ratiba
 yako mwenyewe na uifuate kila siku.
Panga
 kabisa ni muda gani unaamka, ukiamka unafanya nini, muda gani 
unapumzika, unakula na unakuwa na familia. Yote hayo lazima uyapange na 
kisha kuyafuata.
Ukianza siku zako bila mpango, utajikuta umefanya mengi, umechoka lakini hakuna kikubwa ulichokamilisha.
Kwenye ratiba yako ya siku tenga kabisa masaa ambayo huhitaji usumbufu, hayo ni masaa ya kazi zinazohitaji umakini mkubwa.
( 03 ). VAA  KAMA  UNAENDA  KAZINI / SHULENI / CHUONI
Unapofanyia
 kazi nyumbani, una uhuru wa kuvaa utakavyo au hata kutokuvaa kabisa. 
Lakini hilo unapaswa kuwa nalo makini, kwa sababu lina madhara ya 
kisaikolojia kwenye utekelezaji wa majukumu yako ya kazi. Kama umevaa 
nguo za kawaida utajiona kama hauna majukumu makubwa.
Hivyo
 unapaswa kujiandaa vizuri kama vile unaenda kazini  shuleni, chuoni kwa kuvaa kabisa 
nguo zako za kazi na kisha kukaa eneo lako la kazi wakati unafanya kazi.
 Unapovaa nguo kama vile unaenda kazini, akili yako inakupa uzito wa 
kikazi na unatekeleza majukumu yako vizuri. 
( 04 ). WATU  WOTE  WAJUE  RATIBA  YAKO.
Ukishaweka
 ratiba yako ya siku, kila mtu kwenye familia anapaswa kuijua. Na 
waeleze wazi kwamba japokuwa upo nyumbani, lakini pia upo kazini au  unajisomea. Kwa 
muda ule wa kazi, mambo yote hapo nyumbani yanapaswa kuendelea kama vile
 wewe haupo kabisa.
Ule
 muda ambao umetenga usisumbuliwe, usisumbuliwe kweli, labda kwa jambo 
la dharura, ambalo hata kama ungekuwa kazini basi ungepigiwa simu. Na 
weka kabisa vigezo vya dharura ni vipi. Usipofanya hivi, watu watatumia 
uwepo wako kuuliza vitu mbalimbali na hilo kuathiri kazi zako.
Kuhusu
 wageni, kama kuna mgeni amekuja na hukuwa na miadi naye, usikutane naye
 wakati ambao unafanya kazi. Anapaswa kuelezwa ratiba yako na muda mzuri
 kwako kukutana naye. Na kama ni mgeni muhimu, unaweza kumsalimia na 
kumpa ratiba yako ilivyo na mkapanga muda gani mzuri wa kuwa na 
maongezi, kama yapo na ni muhimu.
 ( 05 ). TENGENEZA  MIPAKA YA  KAZI / KUSOMA  NA  MAISHA.
Kwa
 kuwa upo nyumbani na unafanyia kazi nyumbani, mpaka kati ya kazi na 
maisha unafutika kabisa. Wakati wa kazi utaingiliwa na mambo ya 
kifamilia na wakati wa familia utaingiliwa na mambo ya kikazi.
Ni
 lazima utengeneze mpaka kati ya kazi na maisha, ufanye kazi wakati wa 
kazi na maisha wakati wa maisha. Jisukume kutekeleza majukumu yako ya 
kazi kwa wakati uliopanga kufanya kazi na ule wakati uliopanga kupumzika
 au kuwa na familia basi usiruhusu kazi au  masomo kuingilia wakati huo.
( 06 ). TUMIA  VIFAA  VYA  KUONDOA  USUMBUFU.
Kama
 mazingira ya nyumbani kwako siyo rafiki kwako kupata utulivu wa kazi au kusoma, 
labda kuna kelele mbalimbali za majirani na watu wengine, basi tumia 
vifaa vya kuondoa usumbufu.
Hapa
 unapaswa kuwa na spika za masikioni (headphone au earphone) ambazo 
utazivaa wakati wa kufanya kazi. Kuna ambazo zina sifa ya kufunga kelele
 za nje zisikuingie na hivyo kukupa utulivu mkubwa wa kufanya kazi zako.
Pia
 kitendo cha kuvaa spika hizo, kinamfanya mtu asikusemeshe mara kwa 
mara, kwa sababu anajua humsikii. Pia mtu anapokusemesha, jifanye kama 
humsikii, hata kama unamsikia, hasa pale jambo linapokuwa siyo muhimu.
Inayoendana
 na hii ni kuandaa orodha ya nyimbo (playlist) zinazokupa utulivu na 
kuitumia wakati unafanya kazi zako. Hapa unasikiliza nyimbo hizo kwa 
kujirudia rudia na hilo linafanya akili yako izame kwenye kazi 
unayofanya na kuepuka usumbufu.
 ( 07 ). JALI  AFYA  YAKO.
Unapofanyia
 kazi nyumbani, kama kazi zako ni za kutumia akili na unazipenda sana, 
unaweza kujikuta umekaa kwenye kazi siku nzima na hujatoka kabisa nje ya
 nyumba yako. Pia ulaji ni rahisi sana unapokuwa nyumbani kuliko ukiwa 
kazini, ni rahisi kula mara kwa mara ukiwa nyumbani kuliko ukiwa kazini.
Hivyo
 unapaswa kuwa na mkakati wa kujali na kuboresha afya yako. Kitu cha 
kwanza muhimu ni kufanya mazoezi, tenga muda wa kufanya mazoezi ambayo 
yatakutoa jasho. Cha pili ni kudhibiti ulaji, usile kwa sababu kuna kitu
 cha kula, bali kula kwa utaratibu maalumu na kuwa makini na kile 
unachokula. Cha tatu ni muda wa kupumzika, unaweza ukakosa mapumziko 
mazuri japo uko nyumbani na hilo likaathiri afya yako.
 (08 ). PANGILIA  MUDA  UNAOENDANA  NA  WEWE  NA  UNAOEPUKA  USUMBUFU.
Kitu
 kimoja ambacho kimekuwa kinanisaidia sana mimi binafsi kuweza 
kukamilisha sehemu kubwa ya uandishi ni kutenga muda wa uandishi ambao 
unaendana na mimi na pia unaepuka usumbufu.
Huwa
 ninaamka saa kumi kamili asubuhi kila siku na baada ya kufanya tahajudi
 na tafakari kisha kuipangilia siku, kuanzia saa kumi na nusu mpaka saa 
12 kamili huo ni muda wa kuandika tu, sifanyi kingine kwenye muda huo. 
Kwa muda huo, nimekuwa na uwezo wa kuandika kwa kiwango kikubwa sana, 
kwa sababu akili inakuwa na utulivu na hakuna usumbufu, maana watu 
wengine wanakuwa wamelala kwenye muda huo.
Hivyo
 na wewe pangilia majukumu yanayohitaji utulivu na umakini kulingana na 
wewe binafsi na mazingira. Yaani yapange kwenye muda ambao akili yako 
iko vizuri lakini pia hakuna usumbufu wa nje.
Watu
 tumegawanyika kwenye makundi mawili; kuna ambao wanaweza kuamka asubuhi
 na mapema na akili zao zikawa vizuri (early birds) na kuna ambao 
wanachelewa kulala na muda wa usiku ndiyo akili zao zinakuwa vizuri 
(night owls). Jijue wewe uko kundi gani, kisha tenga muda ambao wengine 
wamelala na ufanye kuwa wa kazi.
Mfano
 kama uko vizuri kwenye kuamka asubuhi basi amka asubuhi na mapema sana,
 labda saa tisa au saa kumi na kisha tumia masaa mawili ya kwanza kwenye
 kazi inayohitaji umakini wako na utulivu. Muda huo wengi wanakuwa 
wamelala na hivyo usumbufu unakuwa mdogo.
Na kama unachoelewa kulala basi tenga masaa mawili ya usiku mnene ambapo wengine wamelala na akili yako imetulia kufanya kazi.
Ukiweza
 kutenga masaa mawili ambapo akili yako imetulia na ina umakini na 
hakuna usumbufu wa nje, kisha kuyaweka masaa hayo mawili kwenye kazi, 
utatekeleza majukumu makubwa kuliko anayefanya kazi siku nzima kwenye 
ofisi isiyo na utulivu.
Rafiki
 yangu mpendwa, mdau  wangu  huu ndiyo mwongozo sahihi kwako wa kufanyia kazi 
nyumbani .(  kama  wewe  ni  MWAJIRIWA , UMEJIAJIRI , MWANAFUNZI , MWANACHUO  ni  mwongozo  mzuri  sana  kuufuata.
 
