Monday, April 6, 2020

UMEZALIWA ILI UFANIKIWE / YOU ARE BORN TO SUCCEED. HUFANIKIWI KWA SABABU ZIFUATAZO : --

 Mambo kumi ( 10 ) unayopenda kufanya kila siku, ambayo yanakuzua isifikie ushindi wako :--
( 1 ). HUJACHAGUA  KUWA  MSHINDI.
Hatua ya kwanza kuchukua ili kufikia ushindi kwenye maisha yako, ni kuchagua ushindi unaotaka kwenye maisha yako. Upo usemi kwamba kama hujui unakokwenda, njia yoyote itakuwa sahihi kwako. Hivi ndivyo wengi wanaendesha maisha yao, hawajui wanataka nini, ila wako bize kweli kweli.
Chagua leo unataka ushindi wa aina gani kwenye maisha yako ili uweze kuchukua hatua sahihi za kukufikisha kwenye ushindi huo.
( 2 ). HUJACHUKUA  JUKUMU  LA  MAISHA  YAKO.
Kama umewahi kulalamika au kumlalamikia mtu mwingine juu ya jambo lolote linalohusu maisha yako, basi jua unajizuia kushinda. Washindi wanachukua jukumu la maisha yao kwa asilimia 100. Chochote kinachotokea kwenye maisha yao, wanajua wa kwanza kulaumiwa na kulalamikiwa ni wao wenyewe. Kulalamika na kulaumu ni rahisi, lakini inakufanya ujione usiye na hatia na uwezo wa kupambana kwenye maisha yako.
Amua leo kushika hatamu ya maisha yako, chukua jukumu la maisha yako kwa asilimia 100 kwa kutokulalamika au kumlaumu yeyote.
(3 ). HUAMINI  KWAMBA  UNAWEZA  KUSHINDA / KUFANIKIWA.
Unapokutana na changamoto kidogo, unakata tamaa na kuona safari ya mafanikio haiwezekani. Watu wanapokupinga na kukukosoa unawasikiliza na kuona wapo sahihi kuliko wewe. Na hilo limekuwa kikwazo kwako. Ushindi unataka ujiamini kupitiliza, uamini unaweza kufanya chochote unachopanga, licha ya ugumu au changamoto unazopitia. Na ukweli ni kwamba, ukiamini na kuamua, hakuna kinachoshindikana.
Jiamini kwamba unaweza kushinda, licha ya magumu na changamoto unazopitia, endelea kuweka juhudi na utafikia ushindi mkubwa. 
( 4 ). HUNA  MALENGO  YANAYOPIMIKA.
Dhana yako ya malengo ni potofu, kwa sababu unajiambia tu kwamba mwaka huu nitafanikiwa zaidi, nitaongeza kipato, nitaanzisha biashara na kadhalika. Kujiambia kauli kama hizo siyo malengo, bali ni matamanio. Malengo ni pale unapopanga nini unataka, kwa kiwango gani na kufikia lini. Kama umepanga kuanza biashara, unajiambia kabisa ni biashara ya aina gani na utakuwa umeianza kufikia tarehe gani. Kama huwezi kupima malengo, huwezi kuyafikia.
Weka malengo yanayopimika na kila siku jipime kwa malengo hayo, gawa malengo hayo kwenye hatua za kuchukua na kila siku chukua hatua hizo bila kuacha na utafika kwenye ushindi.
( 5 ) . UMEKOSA   UAMINIFU.
Umekuwa unasikiliza kauli za wale walioshindwa, ambao wanaamini wale waliofanikiwa kuna namna wamefanya. Utawasikia masikini wakisema matajiri ni wezi na walaghai. Utawasikia wasioweka juhudi wakisema waliofanikiwa wana bahati. Wengine wanakuja kwako na njia za mkato za kufanikiwa, ambazo hazihitaji kazi yoyote. Wewe kwa kutokuijua misingi ya mafanikio, unaingia kwenye mitego hiyo, kinachotokea ni unajikuta unapoteza muda wako na hakuna hatua unazopiga.
Chagua kuwa mwaminifu, kufanya kile kilicho sahihi kulingana na misingi ya mafanikio na siyo kudanganyika au kufuata mkumbo. Njia zisizo sahihi zinaweza kukupa ushindi, lakini hautadumu. 
(6). HUWEKI  KAZI.
Umesikiwa watu wanakuambia usifanye kazi kwa nguvu, bali fanya kwa akili, wana kiingereza chao wanakuambia Don’t work hard, work smart. Ni uongo, hakuna ushindi unaopatikana bila kuweka nguvu na akili, tena kwa viwango vya juu sana. Watu wengi ni mashabiki na wafuatiliaji wa michezo mbalimbali. Nitajie mchezaji mmoja unayemkubali sana, ambaye wakati wenzake wanaenda kwenye mazoezi ya nguvu, yeye anafanya mazoezi kwa akili? Hakuna. Halafu wewe unajidanganya kwamba unaweza kufikia ushindi kwa akili bila nguvu!
Amua kuweka kazi, kazi hasa na siyo ya kitoto. Fanya kazi kwa juhudi na maarifa, nenda hatua ya ziada, toa thamani kubwa na ushindi utakuwa wako.
(7 ). HUTHAMINI  MUDA  WAKO.
Unauchukulia muda wako poa sana, unautawanya kama vile una chemchem ya muda isiyo kauka. Unapoteza muda wako wa thamani kwenye mambo yasiyo na mchango wowote kwenye ushindi wako, kwa sababu hujui hata thamani ya muda huo. Unahangaika na habari mbalimbali, umbeya, udaku, maisha ya wengine na mengine mengi. Halafu unakuja kulalamika kwamba huna muda wa kufanya zaidi yale uliyopanga kufanya.
Upe muda wako thamani, jua ni kiasi gani cha kipato unataka kupata, kisha kigawe kwa masaa na jua saa yako moja ina thamani ya shilingi ngapi. Hivyo unapopoteza muda, unajua kabisa ni kiasi gani cha pesa umepoteza.
(8 ). UNASIKILIZA  SANA  HOFU  ZAKO.
Hakuna mtu asiyekuwa na hofu, ila wewe unazisikiliza sana hofu zako, hivyo huthubutu kufanya kitu chochote kipya na kikubwa, kwa sababu unahofia kushindwa. Wanaoshinda wanapata hofu kama zako, lakini wanajua dawa ya hofu ni kufanya. Kuwa na hofu ni kawaida, ila kuzisikiliza hofu zako na kuzifuata ni kuchagua kuukosa ushindi.
Amua leo kuchukua hatua kwenye yale unayohofia, kwa sababu ndiyo yamebeba mafanikio yako na dawa ya hofu ni kufanya unachohofia.
( 9 ). HUJIFUNZI  KILA  SIKU.
Unapata muda wakula mara tatu kwa siku, kufuatilia habari, kufuatilia maisha ya wengine na kulala, lakini unajiambia huna muda wa kusoma vitabu. Hapo ndipo unapoagana na ushindi wako. Kwa sababu hakuna mshindi ambaye hajifunzi kila siku. Moja ya mahitaji ya maisha ya ushindi ni kila siku kuwa bora kuliko siku iliyopita, na ubora pekee utaupata kupitia kujifunza kila siku na kufanyia kazi yale unayojifunza.
Chagua sasa kujifunza kila siku, haijalishi siku yako imebana kiasi gani, hakikisha unatenga muda wa kujifunza kupitia usomaji wa vitabu na mafunzo ya aina nyingine. Usikubali siku ipite hujajifunza kitu kipya.
( 10 ). BADALA  YA  KUZALISHA  MATOKEO , UNAZALISHA  SABABU.
Kabla hata hujaanza kufanya kitu, tayari umeshatengeneza sababu za kujitetea utakaposhindwa kwenye kitu hicho. Hivyo badala ya kuweka nguvu zako kubwa kuzalisha matokeo ya ushindi unayotaka, unapeleka nguvu hizo kuzalisha sababu za kujitetea. Huwezi kuzalisha sababu na matokeo kwa pamoja, chagua kuzalisha sababu na kuachana na matokeo au kuzalisha matokeo na kuachana na sababu.
Kataa kuwa mtu wa sababu, kuwa mtu wa kujisukuma kwa kila namna kupata matokeo unayotaka, usiwe mtu wa kukimbilia sababu.

KISWAHILI---DARASA LA 5, 6 & 7---MAJARIBIO 1---25---MASWALI NA MAJIBU---KWA SHULE ZA MSINGI---TANZANIA---- ( PDF )

Wednesday, March 25, 2020

MWONGOZO WA KUFANYIA KAZI AU KUJISOMEA KWA WANAFUNZI NYUMBANI !!

FAIDA  ZA  KUFANYIA  KAZI  / KUJISOMEA  NYUMBANI.
Kufanyia kazi zako nyumbani, iwe umeajiriwa au umejiajiri au  wewe  ni  mwanafunzi wa  shule  za   msingi , sekondari  au  chuo   kuna faida nyingi sana, baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;
  1. Unaokoa muda mwingi ambao huwa unaupoteza kwa kwenda eneo la kazi, shule au  chuo  Kuanzia muda unaotumia kwenda, kurudi na mwingine unaopotea, kwa kufanyia kazi nyumbani hupotezi muda wako.
  2. Unapunguza fursa za kupoteza muda zinazopatikana kwenye eneo la kazi, mfano mikutano mbalimbali ambayo hufanyika maeneo ya kazi, ambayo kwa sehemu kubwa haina tija.
  3. Unafanya kazi kwa mpango wako bila ya kusumbuliwa na wafanyakazi wengine.Kama  mwanafunzi  au  mwanachuo unaepuka  kelele  za  wanafunzi  wenzako . Japo kunakuwa na mawasiliano ya simu au njia nyingine za mtandao, ile hali ya kukatishwa na wengine wakati unafanya kazi  au  unajisomea  inapungua.
  4. Kwa sehemu kubwa unakuwa na uhuru wa kupanga muda wako mwenyewe, hasa kama kazi yako haihitaji kushirikiana na wengine wakati mnaifanya. Unaweza kupanga kufanya kwa muda unaofaa kwako.
  5. Unapata muda mwingi wa kupumzika, majukumu yako unayofanya ukiwa kazini, shule , chuo ukiyafanyia nyumbani itakuchukua nusu ya muda unaotumia kuyafanya ukiwa kazini , shule  au  chuo .Hivyo unapata muda mwingi wa kupumzika au kufanya mambo mengine.
Changamoto za kufanyia kazi nyumbani.
Hakuna kisichokuwa na changamoto, na katika kufanyia kazi nyumbani, zipo changamoto nyingi. Hapa ni baadhi ya changamoto hizo;
  1. Kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa wakati kwa sababu hakuna anayekusimamia moja kwa moja au anayekuangalia. Unahitaji nidhamu kali sana kuweza kujisimamia mwenyewe.
  2. Usumbufu wa wanafamilia wakati unafanya kazi, wengi hawajui kwamba japo upo nyumbani pia upo kazini, hivyo kuingilia kazi zako pale wanapokuwa na mahitaji mbalimbali.
  3. Kukosekana kwa mipaka kati ya kazi na maisha. Kwa kuwa unafanyia vyote nyumbani, ni rahisi kushindwa kuweka mipaka, ukajikuta unaruhusu mambo ya kifamilia kuingia kwenye wakati wa kazi au mambo ya kikazi kuingia kwenye wakati wa familia.
  4. Wageni usiokuwa na miadi nao wanapokuja nyumbani na kujua upo, wanaingilia sana muda wako wa kazi. Wengi hawawezi kuelewa kwamba japokuwa upo nyumbani, upo kazini, hivyo kuhitaji muda wako mwingi.
  5. Ni rahisi kwa uvivu kukunyemelea, ukipatwa na usingizi kidogo ni rahisi kwenda kulala au kufanya mambo mengine ya kupoteza muda kama kuangalia tv, kuzurura mitandaoni na kadhalika.
MKAKATI  BORA  KWAKO  WA   KUFANYIA  KAZI  NYUMBANI.
Ili kupata manufaa ya kufanyia kazi nyumbani, pamoja na kuzuia changamoto zake zisiwe kikwazo kwako, tengeneza mkakati mzuri kwako kufanyia kazi nyumbani
Zingatia mambo yafuatayo katika kutengeneza mkakati wako wa kufanyia kazi nyumbani utakaokupa matokeo mazuri.
( 01 ). TENGA  ENEO  LA  KUFANYIA  KAZI.
Kitu cha kwanza muhimu kabisa kwako kufanya ni kutenga eneo la kufanyia kazi ukiwa nyumbani. Huwezi kuwa unafanyia kazi kila mahali na ukawa na nidhamu nzuri. Badala yake unapaswa kutenga eneo ambalo utakuwa unafanyia kazi zako, na ukiwa eneo hilo unachofanya ni kazi tu na siyo kitu kingine.
Hii inakuandaa kisaikolojia kuheshimu eneo hilo na unapokuwa kwenye eneo hilo unajua cha kufanya ni kazi. Kama unaishi kwenye nyumba kubwa unaweza kutenga chumba utakachotumia kama ofisi. Lakini kama huwezi kufanya hivyo unaweza kutenga eneo kwenye chumba chochote, hata kile unacholala na kulitumia kama eneo la kazi.
Kama unatenga eneo ndani ya chumba chenye matumizi mengine, hakikisha unaweka kiti na meza kwa ajili ya kufanyia kazi. Hivyo unapokaa kwenye kiti na meza hiyo, unajua kabisa hili ni eneo la kazi. Usifanye kitu kingine unapokuwa kwenye kiti na meza ulivyoandaa kwa ajili ya kazi.
Epuka kufanyia kazi kitandani au kwenye kochi, kwenye maeneo hayo hutaipa kazi uzito kwa sababu kisaikolojia unayachukulia kama maeneo ya kupumzika
 ( 02 ). TENGENEZA  RATIBA  YAKO  YA  KILA  SIKU  NA  IFUATE.
Japokuwa una uhuru wa muda gani ufanye kazi unapokuwa nyumbani, uhuru huo una mipaka. Huwezi kufanya kazi zako pale unapojisikia, ukienda kwa mpango huo hutafanya chochote. Ndiyo una uhuru, lakini lazima utengeneze ratiba yako mwenyewe na uifuate kila siku.
Panga kabisa ni muda gani unaamka, ukiamka unafanya nini, muda gani unapumzika, unakula na unakuwa na familia. Yote hayo lazima uyapange na kisha kuyafuata.
Ukianza siku zako bila mpango, utajikuta umefanya mengi, umechoka lakini hakuna kikubwa ulichokamilisha.
Kwenye ratiba yako ya siku tenga kabisa masaa ambayo huhitaji usumbufu, hayo ni masaa ya kazi zinazohitaji umakini mkubwa.
( 03 ). VAA  KAMA  UNAENDA  KAZINI / SHULENI / CHUONI
Unapofanyia kazi nyumbani, una uhuru wa kuvaa utakavyo au hata kutokuvaa kabisa. Lakini hilo unapaswa kuwa nalo makini, kwa sababu lina madhara ya kisaikolojia kwenye utekelezaji wa majukumu yako ya kazi. Kama umevaa nguo za kawaida utajiona kama hauna majukumu makubwa.
Hivyo unapaswa kujiandaa vizuri kama vile unaenda kazini  shuleni, chuoni kwa kuvaa kabisa nguo zako za kazi na kisha kukaa eneo lako la kazi wakati unafanya kazi. Unapovaa nguo kama vile unaenda kazini, akili yako inakupa uzito wa kikazi na unatekeleza majukumu yako vizuri. 
( 04 ). WATU  WOTE  WAJUE  RATIBA  YAKO.
Ukishaweka ratiba yako ya siku, kila mtu kwenye familia anapaswa kuijua. Na waeleze wazi kwamba japokuwa upo nyumbani, lakini pia upo kazini au  unajisomea. Kwa muda ule wa kazi, mambo yote hapo nyumbani yanapaswa kuendelea kama vile wewe haupo kabisa.
Ule muda ambao umetenga usisumbuliwe, usisumbuliwe kweli, labda kwa jambo la dharura, ambalo hata kama ungekuwa kazini basi ungepigiwa simu. Na weka kabisa vigezo vya dharura ni vipi. Usipofanya hivi, watu watatumia uwepo wako kuuliza vitu mbalimbali na hilo kuathiri kazi zako.
Kuhusu wageni, kama kuna mgeni amekuja na hukuwa na miadi naye, usikutane naye wakati ambao unafanya kazi. Anapaswa kuelezwa ratiba yako na muda mzuri kwako kukutana naye. Na kama ni mgeni muhimu, unaweza kumsalimia na kumpa ratiba yako ilivyo na mkapanga muda gani mzuri wa kuwa na maongezi, kama yapo na ni muhimu.
( 05 ). TENGENEZA  MIPAKA YA  KAZI / KUSOMA  NA  MAISHA.
Kwa kuwa upo nyumbani na unafanyia kazi nyumbani, mpaka kati ya kazi na maisha unafutika kabisa. Wakati wa kazi utaingiliwa na mambo ya kifamilia na wakati wa familia utaingiliwa na mambo ya kikazi.
Ni lazima utengeneze mpaka kati ya kazi na maisha, ufanye kazi wakati wa kazi na maisha wakati wa maisha. Jisukume kutekeleza majukumu yako ya kazi kwa wakati uliopanga kufanya kazi na ule wakati uliopanga kupumzika au kuwa na familia basi usiruhusu kazi au  masomo kuingilia wakati huo.
( 06 ). TUMIA  VIFAA  VYA  KUONDOA  USUMBUFU.
Kama mazingira ya nyumbani kwako siyo rafiki kwako kupata utulivu wa kazi au kusoma, labda kuna kelele mbalimbali za majirani na watu wengine, basi tumia vifaa vya kuondoa usumbufu.
Hapa unapaswa kuwa na spika za masikioni (headphone au earphone) ambazo utazivaa wakati wa kufanya kazi. Kuna ambazo zina sifa ya kufunga kelele za nje zisikuingie na hivyo kukupa utulivu mkubwa wa kufanya kazi zako.
Pia kitendo cha kuvaa spika hizo, kinamfanya mtu asikusemeshe mara kwa mara, kwa sababu anajua humsikii. Pia mtu anapokusemesha, jifanye kama humsikii, hata kama unamsikia, hasa pale jambo linapokuwa siyo muhimu.
Inayoendana na hii ni kuandaa orodha ya nyimbo (playlist) zinazokupa utulivu na kuitumia wakati unafanya kazi zako. Hapa unasikiliza nyimbo hizo kwa kujirudia rudia na hilo linafanya akili yako izame kwenye kazi unayofanya na kuepuka usumbufu.
( 07 ). JALI  AFYA  YAKO.
Unapofanyia kazi nyumbani, kama kazi zako ni za kutumia akili na unazipenda sana, unaweza kujikuta umekaa kwenye kazi siku nzima na hujatoka kabisa nje ya nyumba yako. Pia ulaji ni rahisi sana unapokuwa nyumbani kuliko ukiwa kazini, ni rahisi kula mara kwa mara ukiwa nyumbani kuliko ukiwa kazini.
Hivyo unapaswa kuwa na mkakati wa kujali na kuboresha afya yako. Kitu cha kwanza muhimu ni kufanya mazoezi, tenga muda wa kufanya mazoezi ambayo yatakutoa jasho. Cha pili ni kudhibiti ulaji, usile kwa sababu kuna kitu cha kula, bali kula kwa utaratibu maalumu na kuwa makini na kile unachokula. Cha tatu ni muda wa kupumzika, unaweza ukakosa mapumziko mazuri japo uko nyumbani na hilo likaathiri afya yako.
(08 ). PANGILIA  MUDA  UNAOENDANA  NA  WEWE  NA  UNAOEPUKA  USUMBUFU.
Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinanisaidia sana mimi binafsi kuweza kukamilisha sehemu kubwa ya uandishi ni kutenga muda wa uandishi ambao unaendana na mimi na pia unaepuka usumbufu.
Huwa ninaamka saa kumi kamili asubuhi kila siku na baada ya kufanya tahajudi na tafakari kisha kuipangilia siku, kuanzia saa kumi na nusu mpaka saa 12 kamili huo ni muda wa kuandika tu, sifanyi kingine kwenye muda huo. Kwa muda huo, nimekuwa na uwezo wa kuandika kwa kiwango kikubwa sana, kwa sababu akili inakuwa na utulivu na hakuna usumbufu, maana watu wengine wanakuwa wamelala kwenye muda huo.
Hivyo na wewe pangilia majukumu yanayohitaji utulivu na umakini kulingana na wewe binafsi na mazingira. Yaani yapange kwenye muda ambao akili yako iko vizuri lakini pia hakuna usumbufu wa nje.
Watu tumegawanyika kwenye makundi mawili; kuna ambao wanaweza kuamka asubuhi na mapema na akili zao zikawa vizuri (early birds) na kuna ambao wanachelewa kulala na muda wa usiku ndiyo akili zao zinakuwa vizuri (night owls). Jijue wewe uko kundi gani, kisha tenga muda ambao wengine wamelala na ufanye kuwa wa kazi.
Mfano kama uko vizuri kwenye kuamka asubuhi basi amka asubuhi na mapema sana, labda saa tisa au saa kumi na kisha tumia masaa mawili ya kwanza kwenye kazi inayohitaji umakini wako na utulivu. Muda huo wengi wanakuwa wamelala na hivyo usumbufu unakuwa mdogo.
Na kama unachoelewa kulala basi tenga masaa mawili ya usiku mnene ambapo wengine wamelala na akili yako imetulia kufanya kazi.
Ukiweza kutenga masaa mawili ambapo akili yako imetulia na ina umakini na hakuna usumbufu wa nje, kisha kuyaweka masaa hayo mawili kwenye kazi, utatekeleza majukumu makubwa kuliko anayefanya kazi siku nzima kwenye ofisi isiyo na utulivu.
Rafiki yangu mpendwa, mdau  wangu  huu ndiyo mwongozo sahihi kwako wa kufanyia kazi nyumbani .(  kama  wewe  ni  MWAJIRIWA , UMEJIAJIRI , MWANAFUNZI , MWANACHUO  ni  mwongozo  mzuri  sana  kuufuata.