AN ONLINE PLATFORM THAT PROVIDES EDUCATIONAL CONTENT,SYLLABUSES, STUDY NOTES/ MATERIALS ,PAST PAPERS, QUESTIONS & ANSWERS FOR THE STUDENTS,FORM I--VI ,RESITTERS,QT, ADULT LEARNERS, COLLEGE STUDENTS, PUPILS, TEACHERS, PARENTS,TEACHERS OF THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA AND WORLDWIDE.YOU ARE WELCOME TO SHARE YOUR KNOWLEDGE AND IDEAS.ENJOY MASATU BLOG.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE. "LEARN.REVISE.DISCUSS".Anytime, Anywhere.
- HOME
- UTAKUZAJE UWEZO WAKO WA LUGHA ?
- MBINU ZA KUSOMA NA KUFAULU MITIHANI
- HOW TO IMPROVE YOUR MEMORY
- ONLINE LEARNING & DISTANCE LEARNING ( E--LEA...
- O-LEVEL & A--LEVEL SYLLABUS
- FORM FOUR ( F 4 )--SUBJECTS---TANZANIA
- FORM TWO ( F 2 )--SUBJECTS---TANZANIA
- FORM ONE ( F 1 )-- SUBJECTS---TANZANIA
- FORM FIVE( F 5 ) AND SIX ( F 6 )--SUBJECTS ---TANZANIA
- FORM THREE ( F 3 ) SUBJECTS----TANZANIA
- STANDARD 1 & 2 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA 1 & 2-...
- STANDARD 3 & 4 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA 3 & 4...
- STANDARD 5, 6 & 7 SUBJECTS / MASOMO YA DARASA...
Friday, March 21, 2014
KISWAHILI KIDATO CHA V---VI
TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri [Translation]
Dhana ya Tafsiri.
Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002: 271]
Catford [1965:20] anasema tafsiri ni, “Kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja {lugha chanzi} na kuweka badala yake mawazo yanayolingana katika lugha nyingine {lugha lengwa}.
Vilevile imefasiliwa kuwa ni “Mawazo yaliyotolewa kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.”
TUKI [2002: 271] Tafsiri ni kueleza maana ya maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Maana zote hizo tulizoziangalia, utaona kuwa, kuna mambo matatu muhimu yanayojitokeza, mambo hayo ni:
(i) Mawazo yanayotakiwa kutafsiriwa sharti yawe katika maandishi.
(ii) Mawazo au ujumbe kati ya lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
(iii) Tafsiri inaweza kuwa kutoa maana ya maneno au mawazo.
Baada ya kuangalia maana ya tafsiri, sasa tuangalie maana ya mfasiri na sifa anazotakiwa kuwa nazo mfasiri:
Mfasiri
Mfasiri ni mtu anayefanya tafsiri kutoka lugha moja hadi lugha nyinge.[TUKI:2000:165]
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, mfasiri ni mtu anayehamisha mawazo kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwa kutumia lugha nyingine ili mawazo hayo yaeleweke na watu wasiojua au kuielewa lugha chanzi, na mawazo hayo sharti yawe katika maandishi.
Sifa za mfasiri bora
Mfasiri bora anatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:
? Awe na ujuzi wa lugha fasaha, hii ina maana kuwa awe anajua kwa ufasaha lugha zote mbili, yaani lugha chanzi na lugha lengwa.
? Awe na ufahamu mkamilifu wa ujumbe au mada iliyoandikwa katika matini chanzi na uwezo au jinsi ya kuelezea ujumbe au mada hiyo kwa ufasaha katika lugha lengwa.
? Awe amesoma maandishi ya matini chanzi hadi ayafahamu kinaga ubaga halafu aweze kuyafikiria katika lugha lengwa.
Historia ya Tafsiri nchini Tanzania / Afrika mashariki
Taaluma hii ya tafsiri ina historia ndefu hapa dunia tangu kale, lakini kwa hapa Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla historia hii ya tafsiri haina historia ndefu kwani inaanzia karne ya 19 ambapo wamisionari walitafsiri vitabu mbalimbali vya kikristo ikiwemo biblia kutoka lugha ya kiingereza kwenda Kiswahili na lugha nyingine za makabila makubwa nchini Tanzania.
Na hata wakati wa utawala wa kikoloni hasa waingereza walitafsiri maandiko mbalimbali ya taaluma na fasihi ya Ulaya kwa lugha ya Kiswahili Na hata baada ya uhuru wapo wazalendo waliofanya juhudi za kutafsiri vitabu mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili mfano mzuri ni Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye alitafsiri vitabu viwili vya mwandishi mashuhuri wa tamthiliya wa Uingereza William Shakespeare ambavyo ni: Juliasi Kaizari [1963] na Mabepari wa Venisi[1969] {Tazama pia Mwansoko na wenzake 2006 : 5}
Mfano wa tafsiri ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ni pamoja na ya,Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa ambayo imetafsiriwa na Abdilatif Abdalla, House boy ya Ferdinand Oyono iliyotafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele. Juliasi Kaizari na Mabepari wa Venisiza zaWilliam Shakespeare zilizotafsiriwa na Julius K. Nyerere, Hekaya za Abunuwasi, Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa, Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton na Mashimo ya Mfalme Suleiman kilichotafsiriwa na Sir Rider Haggard, Takadini,kimetafsiriwa na Mathews Bookstore and Stationers, Nitaolewa Nikipenda ambacho kimetafsiriwa na Crement M. Kabugi. vitabu vingine vilivyotafsiriwa ni kama vile; Orodha, Barua Ndefu Kama Hii n.k.
Mpaka sasa wataalamu mbalimbali wamekuwa wakiendelea kutafsiri maandiko mbalimbali kama vile mikataba na ripoti mbalimbali za kimataifa, sheria ambazo mwanzo zilikuwa zikiandikwa kwa lugha ya kiingereza, vitabu vya kiada na ziada, kazi za kifasihi, n.k
Mambo ya kuzingatia katika tafsiri
Katika sehemu hii tutaangalia mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika tafsiri, hivyo basi, tutagawa mambo hayo ya kuzingatia katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri na sehemu ya pili, tutaangalia mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri. Tukianza na:
[a] Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri.
? Kwanza unatakiwa kusoma matini nzima.
Mtu anayetaka kutafsiri matini yoyote ile jambo la msingi la kuzingatia ni kuisoma matini nzima tena kwa umakini ili kuelewa maudhui ya matini chanzi, kuweka alama sehemu za matini zenye utata au zisizoeleweka vizuri, hii itamsaidia kubaini ni aina gani ya marejeo muhimu yatakayomsaidia kutafsiri mfano wa marejeo hayo ni kama kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.
? Unatakiwa kubaini lengo la matini chanzi
Baada ya kuisoma matini chanzi, je! Umeweza kubaini lengo la matini chanzi ni nini? Kubaini lengo la matini kutakusaidia kuweza kutafsiri bila kutofautiana/kukinzana na lengo la matini chanzi, mathalani, matini mbili tofauti zinaweza kueleza jambo lilelile na kutumia data zilezile lakini mtindo wa lugha uliotumika unaweza ukaonesha mitazamo miwili tofauti.
Hebu angalia tamthilia ya Mercant of Venice, iliyoandikwa na William Shakespeare na kutafsiriwa na Mwalimu J.K. Nyerere kwa lugha ya Kiswahili na kuitwa Mabepari wa Venisi, kumbuka kuwa tamthiliya hiyo ingeweza kuitwa pia Wafanyabiashara wa Venisi lakini ukiangalia tafsiri ya kwanza [Ya Mwalimu Nyerere] inatupa hisia hasi wakati ya pili huwezi kupata hisia yoyote.{Mwansoko na wenzake 2006:15}
? Unatakiwa kubaini hadhira/ wasomaji lengwa.
Kabla ya mfasiri hajabaini wasomaji au hadhira ya wasomaji wa matini yake ya tafsiri ni vema kwanza akaibaini hadhira ya matini chanzi na ndipo abaini hadhira/ wasomaji mahususi wa matini yake ya tafsiri, maswali anayotakiwa kujiuliza mfasiri ili aweze kuibaini hadhira ya matini yake ya tafsiri ni: je msomaji wa tafsiri yake ni nani? Ana kiwango gani cha elimu, ni msomi wa kawaida au msomi aliyebobea? Wana umri gani na ni jinsia gani? Je hadhira yake imo katika tabaka gani katika jamii? Baada ya kupata majibu ya maswali hayo, mfasiri atakuwa ameibaini hadhira yake,na hii itamsaidia mfasiri kuamua umbo la matini yake, kama ataamua iwe katika umbo la gazeti, jarida, kijarida, n.k. jambo la kuzingatia umbo la matini ya tafsiri ishabihiane na hadhi ya umbo la matini chanzi. Kwa kuibaini hadhira ya matini lengwa itamsaidia mfasiri kuamua kuirahisisha tafsiri yake au kuifanya iwe ngumu kutegemeana na uwezo wa hadhira ya tafsiri lengwa.
? Unatakiwa kubaini mtindo wa matini chanzi.
Vilevile, mfasiri anatakiwa kujua, matini chanzi imetumia mtindo gani katika kuwasilisha maudhui yake, imetumia mtindo wa kirasimu? Au imetumia mtindo wa kitaaluma? Je imetumia mtindo wa kiuandishi wa habari au mtindo wa kimawasiliano yasiyo rasmi? Je ametumia lugha rasmi au ya mtaani? Na inatakiwa mtindo wa matini chanzi ilingane na ile ya matini lengwa. Tazama mifano ifuatayo:
Kingereza: Please, Sir do no mind it! If I arrive earlier I’ll wait for you
Kiswahili: Mkubwa! Kausha tu! Na kama nitatia maguu mapema,
nitakusikilizia Palepale
Ukiangalia mfano huo, utaona kuwa, mitindo iliyotumika katika sentensi hizo ni mitindo miwili tofauti, katika mfano tuliouangalia katika lugha chanzi, mtindo wa lugha uliotumika ni mtindo rasmi, wakati katika tafsiri [lugha lengwa] mtindo uliotumika ni mtindo wa lugha ya mtaani, jambo ambalo si zuri katika tafsiri. Mtindo wa lugha lengwa sharti ulingane na mtindo wa lugha chanzi.
hivyo katika mfano huo, mtindo sahihi ungetakiwa kuwa;
Tafadhari! usijali! kama nitafika mapema, nitakusubiri.
? Kusoma matini kwa mara ya mwisho
Jambo lingine la kuzingatia ni kuisoma upya matini chanzi. Katika kipengele hiki, mfasiri anashauriwa aisome matini chanzi kwa mara ya mwisho huku akipigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri.
Hayo ndiyo mambo ambayo, mfasiri anatakiwa kuyazingatia kabla hajaanza mchakato wa kutafsiri. Hivyo basi, sasa tugeukie upande wa pili ambao ni:
[b] Mambo ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri.
? Maandalizi ya kutafsiri
Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake, mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri, anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.
? Uchambuzi wa matini chanzi
Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika au kuyapigia mstari katika hatua ya maandalizi na kuyatafutia visawe vyake katika lugha lengwa, hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile, kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.
Mfasiri anatakiwa kuwa na shajara au daftari dogo kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu ya matini chanzi na visawe vyake, visawe vinavyoonekana kufaa viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kuvirejelea wakati wa kutafsiri, vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini chanzi ni ndefu sana, anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo kama vile, sura, aya au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya nyingine.
? Uhawilishaji
Uhawilishaji ni uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au uhamishaji wa mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri. Hii ina maana kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa katika hatua ya uchambuzi huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake.
? Kusawidi /Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri.
Katika hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi, na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake.
? Kudurusu / kuipitia rasimu ya kwanza
Baada ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.
? Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu wengine
Baada ya mfasiri kuipitia rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa makosa yaliyojitokeza, anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu hiyo iliyofanyiwa marekebisho ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo basi wasomaji hao wanaweza wakahakiki,wakashauri, n.k. Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri wenye mantiki.
? Usawidi /Kuandika rasimu ya mwisho
Baada ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho ambayo itakuwa tayari kwa kusomwa na wasomaji.
Njia / mbinu za Tafsiri
Zipo njia mbalimbali ambazo hutumika katika kutafsiri, baadhi ya njia hizo ni kama vile:
(i) Tafsiri ya neno kwa neno. [Word to word translation]
(ii) Tafsiri sisisi.[ Literal translation]
(iii) Tafsiri ya kimaana/uwazi.[ Semantic translation]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano.[Communicative translation]
(i) Tafsiri ya neno kwa neno [Word to word translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha. Katika aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika. Na kwa kawaida matini inayotafsiriwa huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi. Tazama mifano ifuatayo ya tafsiri ya neno kwa neno:
Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi
Kingereza: He/past/study/until/morning
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his
Kiswahili: Anasoma kitabu changu
Kingereza: He/present/book/my
Kiswahili: Walikula chakula chote
Kingereza: They/past/eat/food/all
Umuhimu wa njia hii, humsaidia mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi, kaina hii ya tafsiri hutumiwa na wataalamu wa lugha kuonesha namna maumbo au muundo wa lugha chanzi ulivyo, lakini mapungufu yake ni kuwa, aina hii ya tafsiri huwa haitoi maana inayokusudiwa kwa uwazi zaidi.
(ii) Tafsiri sisisi [ Literal translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: He was taken at the Central Police Station
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.
Badala ya kuwa: Alipelekwa kituo kikuu cha polisi
(iii) Tafsiri ya kisemantiki/maana au uwazi [Semantic Translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Katika aina hii ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani limekosewa haliruhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi katika tanbihi. Sasa tuangalie baadhi ya mifano ya aina hii ya tafsiri:
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza: He went up to hospital
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: Jane alimwoa John
Aina hii ya tafsiri, ina faida kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa kwa kuingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi, mathalani, lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo hiyo ni kama vile:
Kiswahili: Usiku mwema ? kutoka Kingereza: Good night
Kiswhili: Mabibi na mabwana ? kutoka Kingereza: ladies and gentlemen
Kiswahili: Wako mtiifu ? Kutoka Kiingereza: Yours Sincerel
Kiswahili: Naomba nichukue nafasi hii.. ? Kutoka Kiingereza: May I take this opportunity…
[Tazama pia Mwansoko na wenzake: 2006]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano/ huru [Communicative Translation]
Hii ni aina ya tafsiri inayomlenga msomaji [hadhira] wa matini lengwa, ambaye katika aina hii ya tafsiri hatarajii kukutana na ugumu wowote katika matini atakayoisoma, bali hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha yake kwa kadiri itakavyoonekana. Hivyo basi, mfasiri wa aina hii ya tafsiri yuko huru kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno, methali, nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa, pamoja na kuwa tafsiri ya kimawasiliano kufuata sarufi ya lugha lengwa ni lazima pia ifuate utamaduni, mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa. Tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: John alimwoa Jane
Kingereza: No need to cry over spilt milk
Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki
Kiingereza: What comes around goes arround
Kiswahili: Mla vya watu, naye vyake huliwa.
Kiswahili: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
Kiingereza: A friend in need is a friend in need
Kiswahili: Bahati haiji mara mbili
Kiingereza: Golden chance never comes twice
Aina hii ya tafsiri hulenga kutoa athari ile ile au inayokaribiana kwa hadhira ya matini lengwa kama ilivyo kwa hadhira ya matini chanzi[ matini asilia], hii ni aina ya tafsiri ambayo hutumika sana kufasiri mawazo ya kigeni katika lugha na mazingira mapya, mawazo ambayo huelezwa katika misingi ya lugha, utamaduni na mazingira yanayoeleweka kwa hadhira ya matini lengwa.
Ebu tuangalie baadhi ya mifano tuliyoiangalia katika tafsiri ya Kisemantiki [maana] tunavyoweza kutafsiri katika njia ya tafsiri ya kimawasiliano:
Kiingereza Kiswahili
Good night Lala salama
Ladies and Gentlemen Ndugu zangu
Yours Sincerely Ni mimi
May I take this opportunity to… Naomba mnisikilize
Hivyo basi, katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo inayopatikana katika lugha lengwa inayohusiana au kukaribiana na ile ya lugha chanzi. Ebu jaribu kutafsiri misemo/methali zifuatayo ya lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza:
Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
Asiyekubali kushindwa si mshindani
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa
Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Dua la kuku halimpati mwewe
Bandubandu humaliza gogo
Jogoo wa shamba hawiki mjini
La kuvunda halina ubani
Mtegemea cha nduguye hufa masikini
Faida ya aina hii ya tafsiri, humfanya mfasiri kuwa huru kutumia maneno au mafungu ya maneno ambayo huweza kutoa athari ile ile au inayokaribiana na maneno au mafungu ya maneno katika matini ya lugha chanzi, lakini mapungufu ya aina hii ya tafsiri huweza kutokea iwapo mfasiri ataamua kuegemea mno kwenye mawazo, historia, mazingira au itikadi ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: The Merchant of Venice
Kiswahili: Mabepari wa Venisi
Ukiangalia mfano huo utaona kuwa, The Merchant of Venice, tamthiliya iliyoandikwa na William Shakespeare, ingefaa pia kufasiriwa kuwa, Wafanyabiashara wa Venisi, lakini Mwalimu J.K Nyerere aliamua kuifasiri kuwa, Mabepari wa Venisi kutokana na kuwa Nyerere ndiye mwasisi wa itikadi ya Ujamaa nchini Tanzania, hivyo aliegemea katika itikadi kufasiri.
Hivyo basi, mtu anapokuwa anafanya kazi ya kufasiri, maandishi yo yote kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine atajikuta akiangukia katika moja wapo ya njia tulizozijadili hapo juu, lakini ikumbukwe tafsiri ya neno kwa neno ni nadra sana kutumiwa na wafasiri wengi, na njia hizo huweza kuingiliana katika matini moja ya tafsiri.
Ukalimani [Interpritation]
Ukalimani ni nini?
Ukalimani imefasiliwa kuwa ni, uhusishaji wa kuhamisha maana kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa) katika mazungumzo. Hivyo basi tunaweza kusema pia, ukalimani ni hali ya mtu kuhamisha mawazo ya kinachozungumzwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine katika mazungumzo. Hii ina maana kuwa ukalimani ni lazima uhusishe pande mbili, upande wa kwanza sharti awepo mtu anayezungumza lugha fulani na upande mwingine kunakuwa na mtu ambaye anasikiliza hicho kinachozungumzwa na kuyarudia hayo yanayozungumzwa kwa kutumia lugha nyingine tofauti na ile iliyotumiwa na mazungumzaji wa kwanza.
Hivyo basi, ukiangalia, maana hiyo tuliyoiangalia utaona kuwa, ukalimani ni taaluma inayohusu mazungumzo wakati tafsiri yenyewe uhusu maanadishi, kwa maana hiyo huwa tunatafsiri maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine na tunakalimani mazungumzo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Ukalimani ulianza pale ambapo mataifa mbalimbali yenye kuzungumza lugha tofauti tofauti yalipoanza kuingiliana na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa, kichumi na kiutamaduni, kwa mfano ujio wa wageni Afrika Mashariki kama vile Waarabu, Wajerumani na Waingereza ili waweze kuwasiliana na wenyeji wao waliambatana na watu ambao walikuwa wakiwatumia kama wakilamani wao.
Kwa sasa hivi ukalimani umekuwa kama taaluma muhimu, ukalimani unafanyika katika mahakama, kanisani, katika mikutano ya kimataifa, mahubiri ya kidini, n.k na kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna vifaa maalumu ambayo hutumika kukalimani mazungunzo kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, ambayo huvaliwa masikioni katika kumbi za mikutano. Na sasa ni taaluma inayofundishwa katika shule za sekondari na elimu ya juu kama ilivyo kwa tafsiri kutokana na umuhimu wake.
Mkalimani ni mtu muhumi sana katika kufanikisha mawasiliano kwa watu wanaotumia lugha mbili tofauti, au lugha inayotumika katika eneo hilo msikilizaji haielewi na haijui na ndiyo maana utakuta wakalimani wakihitajika mahakamni, mikutano ya kimataifa, katika mahubiri ya kidini au mahali popote pale ambapo wazungumzaji hawawezi kuelewana kwa kuwa wanatumia lugha tofauti.
Sifa za mkalimani bora
? Awe mtu anayezielewa lugha chanzi na lugha lengwa vizuri
? Awe ni mtu ambaye ameishi pande zote za lugha anazozikalimani ili kuelewa mila na desturi za watumiaji wa lugha hizo.
? Awe stadi wa ukalimani, hapa inatakiwa awe na uhodari wa kukalimani, kuzungumza vizuri, maneno kusikika, awe na uwezo wa kukalimani neno kwa neno au sentensi na sentensi, kutumia ishara zinazoambatana na ishara za mzungumzaji wa lugha chanzi na hata kutumia mtindo anaodhani unaweza kuwavutia wasikilizaji wake.
? Muadirifu, ambaye hawezi kupotosha au kubadili ukweli wa kinachozungumzwa, nah ii ni muhimu kwa sababu wakalimani hutumika hadi mahakami hivyo kama si mwadirifu huweza kuufanya upande mmoja ukakosa haki inayostahiri.
? Asiwe mbaguzi, hapa ina maana mkalimani asiamue kupotosha ukweli wa kile kinachozungumzwa kwa kuwa tu kinaendana kinyume na itikadi yake ya kisiasa, kidini, kiutamaduni, n.k. wala asiangalie jinsia ya mtu umri au hali ya mtu anayemfanyia ukalimani.
Mambo ya kuzingatia katika Ukalimani
Kwa ujumla yapo mambo kadha wa kadha, ambayo mkalimani anatakiwa kuyazingatia anapotaka kufanya ukalimani, mambo hayo tunaweza kuyagawa katika makundi mawili, ambayo ni:
1. Kabla ya kuanza ukalimani
Katika hatua hii, mkalimani anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Awe na uelewa mzuri wa lugha zote anazotaka kukalimani, hapa tuna maana kuwa awe na uwezo wa kuzungumza na kuelewa lugha chanzi na lugha lengw, hii itasaidia mkalimani kutopotosha kile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi.
(b) Awe anaijua historia na utamaduni wa jamii zote mbili, yaani ile ya lugha chanzi na ile ya lugha lengwa.
(c) Kama ni ukalimani rasmi, ni vizuri kwa mkalimani akamjua mzungumzaji wa lugha chanzi, ni vema pia ukafanya naye mazungumzo kidogo ili kumzoea, na kutambua vionjo vyake ili iwe rahisi kwa mkalimani pindi atakapokuwa anafanya ukalimani asionekane kama mgeni.
(d) Vilevile ni muhimu kwa mtu anayekalimani, akawa na uelewa mzuri wa mada inayozungumzwa, hii itamrahisishia mkalimani katika ukalimani wake.
2. Katika ukalimani wenyewe
Mkalamani anapokuwa amesimama mbele ya hadhira [wasikilizaji] pamoja na mzungumzaji wa lugha chanzi kwa ajili ya kuanza ukalimani, anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
(a) Kuwa makini katika kusikiliza kile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ili kuepuka kuachwa mahali na kuepuka kumuomba mzungumzaji kurudia mara kwa mara.
(b) Itambue hadhira ya lugha lengwa, ni watu wa namna gani, wana kiwango gani cha elimu, ni wasomi wa kawaida au waliobobea, ni watu wa jinsia na umri gani,? Hii itakusaidi kujua aina ya msamiati na miundo ya tungo utakayoitumia, kama iwe rahisi au migumu kutokana na hadhira yako ilivyo.
(c) Tumia mitindo unayodhani itaeleweka vema na hadhira/ wasikilizaji wa lugha lengwa, kwa mfano kama hadhira yako ni vijana, jaribu kutumia mitindo inayopendwa na vijana, kama wasikilizaji wako ni watu rasmi na we huna budi kuwa rasmi.
(d) Weka mkazo sehemu ambazo mzungumzaji wa lugha chanzi anaweka mkazo ili kuepuka utofauti yako na mzungumzaji wa lugha chanzi, na hata kuepuka kuathiri lengo la mzungumzaji wa lugha chanzi.
(e) Unatakiwa pia kutumia ishara zinazotumiwa na mzungumzaji wa lugha chanzi, hii itawafanya wasikilizaji waamini kile kinachozungumzwa na mzungumzaji wa lugha chanzi ndiyo kilekile kinachozungumzwa na mkalimani.
(f) Usiwe muda mwingi unamtazama mzungumzaji wa lugha chanzi na kusahahu kuitazama hadhira yako, hivyo unatakiwa kuitazama hadhira yako ili kugundua kama wako pamoja na wewe au kuna sehemu hawajakuelewa ili uweze kuwafafanulia zaidi.
(g) Muombe mzungumzaji wa lugha chanzi kurudia sehemu unayodhani hujaisikia au hujaielewa vizuri, kwani ni makosa kwa mkalimani kukalimani sehemu au jambo ambalo hukulisikia vizuri au kulielewa.
Hivyo basi hayo ndiyo mambo muhimu ambayo mkalimani anatakiwa kuyazingatia anapokuwa anafanya ukalimani. Jambo la kuzingatia, mkalimani hutakiwa kuingiza hisia zako unapokuwa anafanya ukalimani. na ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango ambacho mila na desturi zote yaani za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana ama kushabihiana.
Dhima za Tafsiri na Ukalimani
Tafsiri na Ukalimani ina dhima zifuatazo:
? Hutuwezesha kujifunza lugha tofauti.
Kati ya mazoezi mazuri anayoweza kutumia mtu katika kujifunza lugha nyingine, basi zoezi la kutafsiri au kukalimani mara kwa mara humsaidia mtu kujifunza lugha kwa urahisi zaidi, kwani kwa kufanya tafsiri ya mara kwa mara kutamsaidia mtu kugundua miundo na vipengele mbalimbali vya lugha na jinsi vinavyofanya kazi katika lugha anayojifunza.
? Hutumika kama njia ya mawasiliano.
Kutokana na maingiliano ya mataifa mbalimbali yanayotumia lugha tofauti tofauti, tafsiri hutumika kurahisisha mawasiliano baina ya makundi ya watu wanaotumia lugha tofauti tofauti, hutumika kutolea maelezo ya kibiashara kama vile maelekezo ya jinsi ya kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nje au zinazouzwa nje ya nchi, katika matangazo ya kitalii ili kuwavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali, vilevile hutumika katika vyombo vya habari, tafsiri pia inatumika katika nyaraka rasmi, mikataba, vitabu vya ziada na kiada, lakini pia ukalimani hulahisisha mawasiliano miongoni mwa watu wanaozungumza lugha tofauti.
? Tafsiri na Ukalimani hutumika kueneza utamaduni.
Tafsiri imekutanisha lugha na tamaduni mbalimbali duniani na kusababisha tamaduni na lugha hizo kuathiriana, kwa mfano mara baada ya waarabu kuingia Afrika Mashariki na vitabu mbalimbali vya Kiarabu na Kiislamu kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ilisababisha utamaduni wa Kiswahili kuathiriwa na utamaduni wa Kiarabu na Kiislamu kutoka na kuiga kwa mambo mengi kutoka huko, lakini pia hata walipokuja wazungu na kutafsiri vitabu vyao vya kifasihi, kutafsiriwa kwa Biblia, n.k. ilisababisha pia utamaduni wa Mswahili kuathiriwa na utamaduni wa Ulaya.
? Tafsiri na Ukalimani ina dhima ya kuwasilisha ujumbe wa manufaa kwa watu ambao hawafahamu lugha chanzi [lugha asilia]
Changamoto/ mapungufu katika tafsiri na Ukalimani
Mfasiri katika kazi yake ya kufasiri hukumbana na changamoto mbalimbali, ambazo huweza kusababisha tafsiri kuwa na mapungufu ya hapa na pale. Baadhi ya changamoto au mapungufu hayo ni kama vile:
(i) Tofauti za kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.
Tofautui za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza wakati mwingine husababisha matatizo au upungufu katika tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo ya vitenzi vya Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au wingi wa wahusika wala majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa tofauti maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na wingi wa wahusika na hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano ifuatayo kama ilivyotolewa na, Mwansoko [2006]
Kingereza Kiswahili
No parking ? Usiegeshe gari hapa [je kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]
No Smoking ? Usivute sigara[ Je ni sigara tundiyo hairuhusiwi kuvutwa?]
Arrivals ? Wanaowasili
Departures ? Wanaosafiri
Vilevile tofauti za maana kati ya lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani, mathalani:
Kiswahili Kingereza
Wasiojiweza ? Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni walemavu]
[na siyo walimavu wote hawajiwezi]
Wezi wa mifukoni? Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka mifukoni]
(ii) Tofauti za mitindo kati lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za mitindo ya uzungumzaji pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na hii ni kwa sababu unaweza kukuta kuna mitindo fulani inaweza kutumika katika muktadha fulani lakini ikishindwa kupata tafsiri katika lugha nyingine katika muktadha ule ule.mathalani:
Kingereza: Kiswahili
(i) Thou shalt not steal [mtindo wa kidini] ? Usiibe
Do not steal [mtindo wa kawaida] ? Usiibe
(ii) Lend me your ears [mtindo wa kishairi] ? Naomba mnisikilize
May I have your attention [kawaida] ? Naomba mnisikilize
Tafsiri zote tulizoziangalia katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ili ile iliyomo katika matini chanzi lakini tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika katika matini chanzi.
(iii) Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za kiutamaduni, yaani taofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu, kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza wana milo minne wakati Waswahili wana milo mitatu na hii hupelekea kuwa vigumu kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika dhana ya Kiswahili. Mfano:
Waingereza wana: Waswahili wana:
Breakfast ------------------ Kifungua kinywa
Lunch …………………... Chakula cha mchana
High tea ……………………?
Dinner ……………………Chakula cha jioni
Supper …………………….?
Kwa hiyo ukiangalia mifano hiyo, utaona kuwa, high tea na supper kuzipata dhana zake katika lugha ya Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama vile ugali, makande katika lugha ya Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya aina hiyo.
(iv) Tofauti za kiitikadi kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za kiitikadi pia huweza kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwa sababu, utakuta wafasiri wengi hususani waandishi wa habari kuegemea katika itikadi zaidi, kwa mfano:
Kingereza Kiswahili
Bussnessman ? mlanguzi [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi
ya ujamaa]
mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na
itikadi ya ubepari]
Freedom fighter ? wapigania uhuru [Tafsiri ya vyombo vya habari vya
Tanzania wakati wa kupigania uhuru]
Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika
Kusini wakati huo]
Hivyo basi kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango ambacho mila na desturi zote yaana za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana ama kushabihiana.
Na kutokana na umuhimu wa taaluma hii ya tafsiri na ukalimani, serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa Bakita [BAKITA] imeanzisha idara maalumu ya Tafsiri na Ukalimani, na idara hiyo ina majukumu yafuatayo:
? Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mbalimbali kwa masharika, idara, wizara, balozi na watu binafsi.
? Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli za masharika, makampuni na watu binafsi.
? Kupitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na asasi mbalimbali au wafasiri wa nje.
? Kutoa ushauri kuhusu masula ya tafsiri na ukalimani.
MAZOEZI
? Zoezi la kwanza
Fasili matini ifuatayo kwenda lugha ya Kiingereza:
MTO
(Siku ifuatayo, asubuhi. Ngoswe na Mitomingi wako kazini. Wanafika nyumba moja).
MITOMINGI: Hodi! Hodi! Wenyewe! (Kimya, hakuna sauti itokayo). Hodi wenyewe
(Kimya) Labda hawajaamka.
NGOSWE: Kama bado wamelala tuwaache kwanza tuwarudie baadaye.
MITOMINGI: Mimi naona itakuwa shida shida kwani nyumba za hapa zimesambaa
mno.hebu nibishe tena.hodi! hodi! Wenyewe mpo?(Akinyamaza na
kunapita kimya. Punde mlango wafunguka na kipande cha
mwanamke chatokeza). Habari za asubuhi mama?
MAMA: Salama, mwaonaje?
MITOMINGI
NGOSWE Hatujambo
MAMA: Sijui niwasaidie nini akina baba?
MITOMINGI: Mwenyewe yupo sijui?
MAMA: (Akitazama chini mwenye huzuni anatingisha kichwa). Hayupo
MITOMINGI: Katoka kitambo?
MAMA: (Akimtazama Mitomingi kwa jicho kali). Ni marehemu.
MITOMINGI: (Amtazama Ngoswe ambaye kainamisha kichwa na wote wanamtazama
kwa jicho la huruma). Pole mama.
NGOSWE: Pole mama.
MAMA: Nimekwisha poa.
MITOMINGI: Samahani mama , hata sikufahamu.
MAMA: Sio neno baba sio kosa lako.
MITOMINGI: Mungu mkubwa.
MAMA: Nifanyeje; kazi ya Mungu haina dosari. (Ananyamaza kwa kitambo). Je
niwasaidie nini?
MITOMINGI: Jambo moja dogo tu. Samahani kama nitakusumbua maana kwanza ni
asubuhi tena yenyewe ni msiba,
MAMA: Sio kitu baba.
MITOMINGI: Nadhani umepata kumsikia Balozi Mitomingi.
MAMA: Nimemsikia lakini kumwona bado.
MITOMINGI: Basi mama, huyo Mitomingi, Ngengemkeni Mitomingi ndiye mimi.
MAMA: (Kwa mshangao): Karibuni ndani mpumzike
MITOMINGI: Hatukai sana mama.
MAMA: Basi ngoja niwatolee viti make. (Aingia ndani na kutoka na viti viwili
kuwapatia wageni. Yeye aketi chini).
MITOMINGI: Mama!
MAMA: Baba!
MITOMINGI: Nadhani una habari juu ya kuhesabu watu.
MAMA: (Kwa mshangao): Kuhesabu watu?
MITOMINGI: Ndiyo kuhesabu watu.
MAMA: Kuhesabu watu! (Akitingisha kichwa) Hapana.
MITOMINGI: Balozi wenu hakuwajulisha?
MAMA: Hata kidogo.
MITOMINGI: Kweli?
MAMA: Kwani Tambitambi naye mtu yule!
Pombe na yeye ni pete na chanda!
Hajali Balozi wake wala nyumba yake.
MITOMINGI: Ni sawa usemayo mama. Tambitambi yule akili hazimtoshi. Tumefika
kwake wala hajulikani aliko!
MAMA: Kama kuna wanaume mabwege yule ametia for a.
MITOMINGI: Usizidi kunambia mama, Tambitambi mambo yake hakuna
asiyeyafahamu…. Sasa mama!....
MAMA: Ndiyo baba.
MTOMINGI: Sisi kama utuonavyo tuko shughulini, shughuli hiyo si nyingine bali hiyo
niliyoisema sasa hivi kuhesabu watu. Na huyu kijana ndiye karani
mwenyewe ahusikaye. Ingekuwa bora kama wewe na wanao wote
mngetoka nje ili tufanye kazi yetu.
MAMA: Sasa baba mbona itakuwa vigumu.
MITOMINGI: Kwa vipi?
MAMA: Sasa baba utahesabu vipi?
MITOMINGI: Kwa nini?
MAMA: Kama utatuhesabu wewe basi u mchawi.
MITOMINGI: Mbona sikuelewi!
MAMA: Mchawi ndiye anayehesabu watoto wa wenzake ili awaroge. Sasa wewe
umchawi? Hata kama u mchawi siwezi kukubali utuhesabui maana
siwezi kujua nia yako ni mbaya au nzuri.
MITOMINGI: Mtu akuwaniae uovu haji kweupe.
MAMA: Sawa usemayo baba.
NGOSWE: Sasa mama hebu walete wanao na yeyote yule aliye ndani.
MAMA: Wanangu hawapo wamekwenda shamba kuwania mpunga.
NGOSWE: Wote?
MAMA: Ndiyo.
NGOSWE: Ndio kusema hakuna kiumbe hata kimoja?
MAMA; Yuko mke mwenzangu.
NGOSWE; Tuitie.(Mama anasimama kwa unyonge na kuingia ndani. Anarudi peke
yake baada ya muda mfupi). Yu wapi?
MAMA: Aja (Punde mama mwingine atokea. Yu kariby rika moja na mama wa
kwanza isipokuwa huyu mbichimbichi).
MITOMINGI: Habari mama?
NGOSWE: (Wakati huohuo) Shikamoo.
MAMA WA PILI: Nzuri (Atazama chini kwa aibu huku akiketi).
NGOSWE: (Akimtazama mama wa kwanza). Basi; hakuna mtu mwingine ndani?
MAMA WA PILI: (Akikataa kwa kichwa)
MITOMINGI: (Kwa mama wa kwanza). Lakini nyie wanawake mbona waoga sana!
Hivyo mnataka kuniambia motto wa mgongoni anaweza kwenda
kuwania mpunga? (Mama agutuka). Hebu niambie mwanao mchanga
yu wapi?
MAMA WA KWANZA: Sina mtoto mchanga.
MITOMINGI: Hivyo mama wasema kweli?
MAMA WA KWANZA: Haki vile.(Mara kwasikika sauti ya mtoto akilia ndani ya
nyumba).
MITOMINGI: Na huyo anayelia kama si mtoto ni nini/ (Mama ainuka wakawaka na
kuingia ndani kwa aibu. Muda wapiti na harudi). Mama! Njoo basi
tumalize shughuli. Usijali mambo ya motto kulia, ni jambo la kawaida.
(Mama atokea amepakata mtoto mchanga. Aketi chini na sasa uso wake
umejaa hasira na chuki)…
[Imenukuliwa kutoka, Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. Uk 13-15]
? Zoezi la pili
1. Linganisha na linganua kati ya taaluma ya tafsiri na ukalimani.
2. (a) Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiingereza
(i) Dua la kuku halimpati mwewe
(ii) Bandu bandu humaliza gogo
(iii) La kuvunda halina ubani
(iv) Mla vya watu naye vyake huliwa
(v) Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwa nini?
??Zoezi la tatu
1. [a] Kwa kutumia mifano, fafanua istilahi zifuatazo:
[i] Matini chanzi
[ii] Matini lengwa
[iii] Lugha chanzi
[iv] Lugha lengwa
[b] Tafsiri sentensi zifuatazo kwenda lugha ya Kiswahili
(i) All that glister is not gold
(ii) Looser casn't be a chooser
(iii) When you make your bed you must lie on it
(iv) There is no incense for something rotting
(v) When in Rome do, do as Romans do
(b) Ni njia gani umetumia katika tafsiri hizo ulizotoa hapo juu, unadhani ni kwanini?
2. "Mfasiri au mkalimani hukabiliana na changamoto mbalimbali katika kufanikisha kazi
yake." Huku ukitumia mifano thibitisha kauli hiyo.
MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2011
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2011
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2011
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman

Subscribe to:
Posts (Atom)