TAMTHILIA
Tamthilia ni nini?
- Tamthilia ni utanzu ambao
hutegemea mazungumzo na uigizaji ili kuwasilisha ujumbe wake. Huu ni utanzu
ambao huandikwa kwa mtindo wa mazungumzo ya wahusika (Wamitila, 2007).
- Nkwera (h.t) anaelezea kuwa
tamthilia ni: “Tamthilia ni mchezo wa kuigiza au utungo wa
kisanaa ambao huweka wazo fulani katika matendo na mazungumzo” (Nkwera, h.t)
AINA ZA TAMTHILIA
- Kwa mujibu wa Aristotle,
kuna aina mbili za tamthilia. Aina ya kwanza ni tanzia na nyingine ni ramsa.
Tanzia
ni kinyume cha ramsa kwa maana kuwa hutumika kuonesha kuanguka na kushindwa kwa
mhusika maarufu, mbabe, au shujaa atokaye katika tabaka la juu yaani mtu wa
nasaba bora (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234).
Kama
ilivyo kwa ramsa, tanzia ilianzia katika miviga ya kidini, katika sherehe ya
kumhusu Dionisius. Wachezaji na Waigizaji walivalia na kuonekana kama mbuzi
wakiimba nyimbo zilizohusu anguko la shujaa (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya
SW 234).
ARISTOTLE TANZIA ANAONA KUWA; Tanzia ni usanii
uoneshao anguko la mtu ambaye kimsingi ni mwema, shujaa au mbabe kutokana na kosa
la kufisha au kutokana na uamuzi mbaya ambao matokeo yake ni mateso (Mutembei,
2005 katika mihadhara ya SW 234).
Jambo hili linapompata shujaa huyo, jamii nzima huingia katika woga na
kuhangaika kwa hali ya juu, kwani kiongozi wao yumo katika mateso na ni uchuro
wa kufisha jamii kama hatua madhubuti hazitachukuliwa (Mutembei,
2005 katika mihadhara ya SW 234)
MISINGI YA UTOKEAJI WA TANZIA:
Kwa
mujibu wa Mutembei, (kashatajwa) katika mihadhara ya SW 234 anasema kuwa,
misingi ya utokeajiwa tanzia inapaswa izingatie yafuatayo:
- Iwe na
uwezo wa kuamsha hisia za woga na huruma miongoni mwa hadhira.
- Shujaa au
mbabe apataye mkasa ni lazima awe mwema na mwenye kuvutia kwa sura/umbo zuri.
- Watazamaji
huonesha kuumia, husikitika nk. kadri mtu anavyoonekana ni mwema au mzuri wa
umbo lake kama ilivyokuwa kwa mhusika wa Second Chance – Salvado Solenza.
- Katika
Tanzia, anguko la shujaa huja kutokana na ama uamuzi wake mbaya au kosa lake
mwenyewe. Aristotle: alisema kuwa, hakuna kosa la bahati mbaya. Kila mkasa wa
kufisha ni matokeo ya maamuzi mabaya, au kosa fulani.
ISTILAHI KATIKA TANZIA:
HUBRISI- Dhambi yenyewe. Kitendo
chenyewe akitendacho shujaa ambacho humwingiza katika hamartia.
ANAGNORISIS-
Utambuzi wa ndani. Ni ile saa ambapo shujaa hupata utambuzi wa ndani katika
akili ya shujaa ambao humjulisha kuwa kakosea na tayari kesha jitumbukiza
katika anguko kuu. (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
PERIPATEA-Matendo
muhimu ambayo humtoa shujaa katika hali iliyoonekana kuwa afadhali kumdidimiza
katika hali mbaya kabisa. (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
NEMESIS-
Adhabu ambayo haina budi kuwapo kutokana na matendo ya Hubrisi (Mutembei, 2005
katika mihadhara ya SW 234).
Ni aina ya tamthilia ambayo hadhira
inapoangalia isiogope au kupata uchungu bali icheke kwa kumkejeli mhusika
kutokana na matendo yasiyofurahisha katika jamii. Mhusika anatakiwa amfanye
matendo au tabia ambazo ni kinyume na maadili ya jamii, ili yanapomkuta
masahibu – hadhira Imcheke kwa upumbavu na uzembe wake. Mfano mzuri ni mikasa
inayoonesha baadhi ya wanandoa kutokuwa waaminifu katika ndoa zao –
wanapokumbwa na fumanizi na kuumbuka, hadhira itamcheka mhusika kwa kuwa ayafanyayo
hayakubaliki katika maadili. Vilevile aina hii ya tamthilia huishia na mwisho
wa kufurahisha.
SHUJAA WA KI-RAMSA
Kwa
mujibu wa (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234), shujaa wa kiramsa
ni mtu mwenye
sifa zifuatazo:
- Sio
lazima awe mtu maarufu au Mbabe/Shujaa anaweza kuwa ni kichaa au mwendawazimu
fulani ambaye yuko katika jamii
- Mtu
ambaye katika jamii huwa duni, na matendo yake ni ya kiucheshi-ucheshi, ila
historia humlea na kumkuza hata akatokea kuwa “fulani” – akaishi raha
mustarehe.
- Mhusika
ambaye akifanikiwa kila mtu atafurahia na baada ya igizo atakuwa ameridhishwa
na mwisho huo mzuri wa kuishi raha mustarehe.
UHUSIKA WA WAHUSIKA WA KI-RAMSA
- Ramsa
huwahusu watu wa kawaida ambao wana kipato cha kati na chini kama vile: washona
viatu, wauza mitumba, wakata nyama, wachoma mishikaki, wanafunzi, walimu,
wasukuma mikokoteni, n.k. Ramsa haihusu watu wa juu ambao ni kama vile:
wafalme, malkia, viongozi, watu wote wa nasaba BORA (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234)
- Ramsa huhusika na
mambo ya kawaida yanayowahusu watu wa kawaida katika maisha ya kila siku
(Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Mambo kama: Kupata rafiki mpya (au
Kumrudisha wa zamani) au kupata kazi au kupanda cheo kwa mfano akina Mkwere
kwenye Mizengwe kila Jumapili saa tatu usiku, kituo cha ITV.
DHAMIRA ZA
KI-RAMSA
Ramsa huhusika na
mambo ya kawaida yanayowahusu watu wa kawaida katika maisha ya kila siku
(Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Mambo kama: Kupata rafiki mpya (au
Kumrudisha wa zamani) au kupata kazi au kupanda cheo kwa mfano akina Mkwere
kwenye Mizengwe/Ucheshi kila Jumapili saa tatu usiku, kituo cha ITV.
AINA
ZA RAMSA:
UTANI/VICHEKESHO (farce)
Huonekana ni upuuzi, mambo hugeuzwa kinyume.
Sura za wahusika hubadilishwa - kama vinyago. Lengo ni kuchekesha na ndimo
maana yake hupatikana. Mfano tunaweza kuziweka kazi za Mzee Majuto katika aina
hii japo sio sifa zote za utani zinajitokeza katika kazi zao
MAHABA/MAPENZI (romance)
Wapendanao, huwekewa
vikwazo (pesa, kabila, hadhi) lakini hatimaye hushinda vikwazo hivyo. Hupendana
na kuoana (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Tazama kazi nyingi za
filamu hapa nyumbani zinaangukia katika kundi hili; mfano ni Sandra, Johari, Sikitiko langu The Game of Love kwa kuzitaja kwa uchache.
TASHTITI/ DHIHAKA-
(satire) ni zile kazi zinazolenga kuwasilisha dhihaka kwa
viongozi, siasa, au dini (Mutembei, 2005 katika mihadhara ya SW 234). Kwa mfano
zamani Ze Comedy ilipokuwa ikirusha vipindi vyake kupitia East Africa
Television (EATV); kwa sasa wanatambulikana kama Origino Komedà ila wamepwaya katika uwasilishaji wao – sio kama
zamani. Nadhani kuna udhibiti ndani yake.
- Pia
tashititi hizi huhusisha kuakisi yafanywayo na wahalifu, matapeli, wanafiki,
wala rushwa, wafanya magendo, waongo n.k. Mfano ni Bongo Darisalaam kilichokuwa kinachorushwa na TBC1.
- Mhusika
mkuu (ambaye ni Kiongozi) huwa na sifa hizo hapo juu na anadhihakiwa ili aache
rushwa, uhalifu, utapeli, nk.
- Ramsa
hizi ni kama – njia ya walala hoi kutoa malalamiko yao kwa viongozi wao kwa
mfano angalia kazi za Futuhi inayorushwa na Kituo cha Utangazaji cha Star Tv kila
Alhamisi usiku saa tatu.
VIPENGELE VYA TAMTHILIA
- Vipengele vya kifani katika
tamthilia ni pamoja na: wahusika, mtindo, muundo, mandhari, jina la kazi, na
matumizi ya lugha.
VIPENGELE VYA SANAA ZA MAONESHO
Vipengele vya sanaa za maonesho kwa mujibu wa
Aristotle na Semzaba ni hivi vifuatavyo: uhusika na wahusika, maudhui, msuko wa
matukio, uteuzi wa lugha, kionwa, na muziki.
Vipengele hivi vya sanaa za maonesho vimejadiliwa
katika kitini cha Uandishi wa Kubuni kwa Kiswahili Nadharia na Vitendo kilichoandikwa
na Mahenge, E. Soma vipengele hivyo na uvitumie katika kuhakiki kazi za sanaa
za maonesho.
MAUDHUI YA TAMTHILIA
- Maudhui ya tamthilia
yanagusia vipengele vya: migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo, msimamo, na
dhamira.
- Matumizi ya tamthilia ni
pamoja na: kuelimisha jamii; (katika masuala mbalimbali kama vile: uchumi,
siasa, maadili, nk.) kuburudisha jamii, kuonya na kukosoa jamii, kukuza lugha,
kurithisha amali za jamii (mila na desturi za jamii husika), nk.
No comments:
Post a Comment