SINTAKSIA.
MIKABALA YA
TAALUMA YA SARUFI.
(a)
Sarufi ubongo
(b)
Sarufi kama kaida za
kiisimu.
(c) Sarufi kama tafiti na
uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
UTANGULIZI
WETU UTAZINGATIA MAMBO YAFUATAYO
·
Maana
ya sarufi.
·
Mkabala
wa kimapokeo.
·
Mkabala
wa kisasa.
MJADALA
WETU UTAJIKITA KATIKA VIPENGELE VIFUATAVYO
·
Ufafanuzi
wa sarufi ubongo
·
Ufafanuzi
wa sarufi kama kaida za kiisimu
· Ufafanuzi
wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
·
Tofauti
zilizopo katika mikabala hii.
Katika mjadala huu, kwanza kabisa tutaanza kwa kuangalia dhana muhimu ambazo
zimejitokeza katika mada yetu, ambazo ni sarufi, mkabala wa kimapokeo pamoja
na mkabala wa kisasa. Kisha tutangalia kwa kujadili kiini cha mada, ambapo
tutaangalia jinsi sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu na sarufi kama tafiti
na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha na inaangukia katika mkabala
upi na inatofautiana vipi.
Tukianza
na maana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile:-
Kihore
na wenzake (2005) wakimnukuu Gaynor (1968:88), wanaeleza kuwa sarufi ni sayansi
ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida
hukubalika kwa watumiaji wake.
Vile
vile Mdee (1999) anafasili sarufi kama mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha
mzungumzaji kutunga sentensi nyingi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa
lugha.
Pia
Massamba na wenzake (1999:31) katika mtazamo wa pili wa kufasili dhana ya
sarufi wanaeleza kuwa sarufi ni kanuni sheria au taratibu za uchambuzi
zinazotawala lugha.
Hivyo
basi wanasarufi hawa wanaonekana kukubaliana kwamba sarufi ni kanuni, sheria na
taratibu zinazotawala lugha. Lakini kwa kiasi kikubwa tunakubaliana na fasili
iliyotolewa na Mdee kutokana na kwamba ameweza kutufafanulia vizuri kanuni hizo
na taratibu za lugha ndizo zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi nyingi,
sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha.
Kwa
mfano:- sentensi za kiswahili zina muundo wa
N + V + T + E
Mtoto mzuri anacheza uwanjani.
N
V T E
Baada
ya kuangalia dhana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali sasa tunaweza
kuangalia mikabala mikuu miwili ya sarufi ambayo ni:-
i.
Mkabala wa kimapokeo
ii.
Mkabala wa kisasa.
Kwa
kuanza na mkabala wa kimapokeo kwa mujibu Khamisi na Kiango (2002), wanaeleza
kuwa hii ni sarufi ya kale, wataalamu wanaohusishwa na mkabala huu walijitokeza
kuanzia karne ya 5 kabla ya kristo na katika karne ya 18 na karne ya 19 baada
ya kristo, wataalamu hao ni kama vile Plato, Aristotle, Panin, Protagoras ambao
walijihusisha na lugha kwa kutaka kujua asili yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi
wa asili ya maumbo hususani walitaka kujua kama lugha ni tukio la maumbile au
tukio la unasibu.
Pia
Massamba na wenzake (wameshatajwa) wanaeleza kwamba sarufi mapokeo zilikuwa ni
sarufi elekezi ambazo zilisisitiza kanuni na nini cha kusema na wajua lugha.
Watu wasiojua kanuni za lugha wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanaojua sarufi ya
lugha. Wanaendelea kusema kuwa, wanaojua lugha hupaswa kutunga kanuni za
sarufi.
Vile
vile Habwe na Karanja (2004:124), wanadai kuwa mitazamo hii ya wanasarufi hawa
wa kimapokeo iliathiri mbinu na njia za kuangalia lugha kwani sarufi mapokeo
ilijikita katika lugha za kiulaya kama vile kiyunani na kilatini.
Sifa
mbalimbali za lugha hizi ambazo ziliaminiwa kuwa bora, zilichunguza kilatini na
kiyunani zilielezwa kuwa ni lugha duni na kutwezwa na kudhalilishwa
Sarufi
mapokeo ilielekeza watu jinsi ya kutumia lugha, uelekezi huo hata hivyo
ulijikita kwenye sheria za lugha ya kilatini kwa mfano sentensi haikupaswa
kuishia na kihusishi wala kuanza na kiunganishi.
Udhaifu
mkubwa wa sarufi mapokeo ni kwamba, taratibu za uchanganuzi wa lugha
hazikuzingatia lugha ya kuzungumza kama ilivyo leo. Wanasarufi mapokeo walienzi
na kuchunguza lugha ya maandishi. Hivyo basi ni dhahiri kwamba mkabala huu
unaangukia katika mitazamo ya kifalsafa.
Hivyo
basi ni wazi kuwa katika sarufi hii ya mapokeo tunakutana na mikabala miwili
inayoangukia katika mkabala huu ambayo ni sarufi ubongo na sarufi kama kaida za
kiisimu.
Mkabala
wa pili, ni mkabala wa kisasa, unaoongozwa na wanasosiolojia ambao unahusisha
sarufi mbalimbali kama vile :-
i.
Sarufi msonge
ii.
Sarufi miundo virai
iii.
Sarufi geuza maumbo zalishi
iv.
Sarufi husiano
Katika
mkabala huu ndipo tunapata mkabala wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo
inavyooneka kwenye lugha.
Hivyo
basi baada ya kujadili mikabala mikuu miwili ambayo ni mkabala wa kimapokeo na
mkabala wa kisasa, zifuatazo ni sifa muhimu za sarufi ubongo, sarufi kama kaida
za kiisimu na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye
lugha ambazo kwazo tutaona jinsi kila moja inavyotofautiana na nyingine.
Kwa
kuanza na sarufi ubongo, kwa mujibu wa Nordquist (2012), anaeleza kuwa sarufi
ubongo ni sarufi endelevu ambayo inamwezesha binadamu kuzalisha lugha ambayo
inaweza kueleweka kwa wengine
Pia
Sharpe (2006), anaeleza kuwa sarufi hii hufananishwa na umilisi, anaendelea
kueleza kuwa sarufi hii humwezesha mtu kuweza kusikia na kutambua kama sentensi
hiyo ni sahihi au si sahihi.
Chomsky
(1957), anaeleza kuwa kila binadamu amezaliwa na uwezo wa kuzalisha tungo mbalimbali
zisizo na ukomo ambazo humpatia uwezo au uzoefu wa sarufi ya lugha. Pia
anafafanua kwamba kila binadamu huzaliwa na kifaa katika ubongo wake ambacho
kinamwezesha kuamili lugha ya aina yoyote, amekiita kifaa cha uamiliaji lugha
(KIULU). Kwa mfano mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka saba anaweza kuamili
lugha yoyote na mahali popote.
Mgullu
(1999), anaeleza kuwa sarufi ubongo huchunguza jinsi binadamu anavyojifunza
lugha kwa mfano hatua mbalimbali ambazo hupitia wakati anajifunza lugha yake ya
kwanza.
Kwa
hiyo tunakubaliana na fasili zote zilizotolewa na wataalamu hapo juu kutokana
na kwamba sarufi ubongo, hii ni sarufi ambayo inachunguza jinsi binadamu
anavyoweza kuamili lugha na kujifunza lugha pia kuweza kuzalisha sentensi
mbalimbali ambazo anaweza kuzitumia katika mawasiliano.
Vile
vile wataalamu wa mkabala huu hueleza kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya akili,
kufikiri na lugha bila shaka uhusiano huu ni ule wa taathira ya lugha yaani dhana
inayoeleza kuwa kwa kawaida kila lugha huathiri watumiaji wake kwa kiasi
kikubwa.
Vile
vile wataalamu wa mkabala huu wanaeleza jinsi watu wanavyojifunza lugha ya pili
au lugha ya tatu.
Kwa
kifupi mkabala huu hujihusisha na mambo kadha kama vile:-
(i) Kumwezesha binadamu kuweza
kuzalisha au kutunga sentensi mbalimbali.
(ii) Sarufi ubongo huusika na
uamiliaji wa lugha na ujifunzaji wa lugha.
(iii) Sarufi hii huwakilisha
maarifa ya mzungumzaji wa lugha (umilisi alionao mzungumzaji).
Mkabala
mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa sarufi mapokeo ni sarufi
kama kaida za kiisimu.
Kwa
mujibu wa Encyclopedia (1970), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mpangilio
unaoonyesha au kueleza kanuni za kisarufi katika lugha ambazo hushughulika na
kanuni za uundaji wa maneno, maumbo ya maneno, miundo ya maneno, miundo ya
sentensi, vile vile inahusisha taarifa maalumu kuhusu fonetiki na fonolojia
(taaluma inayohusika na utamkaji sahihi unaokubalika)
Pia
kwa mujibu wa Babylon Dictionary (1997), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mfumo
wa kisarufi ambao unafafanua kipi sahihi na kipi si sahihi katika lugha, pindi
mzungumzaji anapozungumza, amezungumza sahihi au si sahihi.
Kwa
hiyo tunaweza kueleza kuwa sarufi kaida hujishughulisha sana na:-
i. Kuelekeza namna ya matumizi
sahihi ya lugha.
ii. Wataalamu wa lugha ndio
wanaounda kanuni na miongozo ya lugha ambayo inatakiwa kufuatwa na wale
wasiojua lugha.
Kwa mfano:- kanuni
mojawapo ya miundo ya sentensi za Kiswahili huwa na muundo wa kiima na kiarifu.
Vile vile sentensi nyingi za
Kiswahili huwa na muundo wa kirai nomino na kirai kitenzi.
Hivyo
basi katika mkabala huu wa sarufi watu wasiojua lugha wanapaswa kufuata kanuni
na taratibu zilizoundwa na wanaojua lugha kwa mfano wanasarufi.
Pia
mkabala mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa kisasa ni sarufi
kama utafiti na uchambuzi wa miundo inayoonekana katika lugha.
Kwa
mujibu wa Besha (2007), anaeleza kuwa huu ni mkabala unaohusika hasa na
uchambuzi wa muundo wa lugha, sauti za lugha, muundo wa sentensi na hata maana
za tungo za lugha.
Pia
mgullu (1999), anaeleza kuwa lengo la mkabala huu ni kufafanua vipengele vyote
vya lugha fulani kama vilivyo hivi sasa au vilivyokuwa wakati fulani.
Hivyo
basi Besha na Mgullu wanakubaliana kuwa huu ni mkabala unaofafanua namna au
jinsi watu wanavyozungumza lugha na sio kuwaelekeza waizungumze vipi lugha
yao.
Hivyo
basi kwa ujumla mkabala huu unajihusisha na mamba yafuatayo:-
i.
Hautilii mkazo mabadiliko
yaliyotokea katika lugha hata kama mabasiliko hayo yapo.
ii.
Mkabala huu hauamuru watu
waseme vipi na vipi wasiseme.
Kutokana
na sifa mbalimbali zilizojitokeza katika mikabala hii, tumeweza kubaini tofauti
zilizopo baina ya mikabala hii mitatu ambazo ni kama zifuatazo:-
Sarufi
ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu zinajitokeza katika mkabala wa kimapokeo
wakati sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha
inajitokeza katika mkabala wa kisasa.
Vilevile
sarufi ubongo humwezesha binadamu kuweza kuzalisha miundo mbalimbali ya tungo
wakati sarufi kama kaida za kiisimu haijihusishi kabisa na masuala ya ubongo
bali yenyewe hujihusisha na mazoea ya kawaida ya watumiaji wa lugha ambapo
kunakuwa na makosa ambayo huwafanya wataalamu kuunda kanuni za lugha ambazo
zinatakiwa kufuatwa na wasiojua lugha hii inatofautiana na sarufi kama tafiti
na uchambuzi wa miundo inavyoonekana kwenye lugha kwa kuwa haihusiani na
masuala ya ubongo wala kaida, bali yenyewe hujihusisha na utafiti na ufafanuzi
wa miundo ya lugha kama inavyotumika na wazungumzaji wa lugha na haiwaelekezi
jinsi ya kuzungumza.
Kwa
kuhitimisha tunaweza kusema kwamba pamoja na tofauti hizo zilizojitokeza katika
mikabala hiyo mitatu, mikabala hii inaonekana kufanana kwani yote inajihusisha
na lugha ya binadamu, pia mikabala hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika
maendeleo ya taaluma ya isimu na ndio imekuwa darajia kwa wataalamu mbalimbali
katika kufanya tafiti zao kwa mfano baada ya kushindwa kwa sarufi ubongo na
sarufi kama kaida za kiisimu ndipo kukazaliwa kwa sarufi kama tafiti na
uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
MAREJEO
Babylon
Dictionary. (1997). Translation and
Information Platform. Babylon Ltd.
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa lugha na Isimu. Macmillan
Aidan Ltd. Dar es Salaam.
Chomsky, N. (1957). Syntactic Structures. Mouton The Hague.
Khamis, A.M na John
G.K (2002). Uchanganuzi wa sarufi ya
Kiswahili. TUKI. Dar es salaam.
Habwe, J na Peter K
(2007). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix
Publishers. Nairobi.
Kihore, Y.M na wenzake. (2008). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA):Sekondari na Vyuo.
TUKI. Dar es Salaam.
Massamba, D.P.B. na
wenzake. (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili
Sanifu (SAMIKISA): Sekondari na Vyuo. TUKI.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na
Mofolojia ya Kiswahili. Longhorn Publishers Ltd. Nairobi.
Sharpe J. P (2006). Barron’s How to prepare for the TOEFL IBT.
Barron’s Educational Series.
The Great Soviet Encyclopedia.
(1970). (3rd ). The Gale group. Moscow.